SERIKALI YAJIPANGA KIKAMILIFU KUPAMBANA NA MAGONJWA YA MIFUGO

Mwakilishi wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Nazaeli Madalla, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha sekta ya mifugo inachangia ipasavyo katika uchumi wa taifa, ikiwemo kupitia kampeni kubwa ya uchanjaji wa mifugo inayofanyika kitaifa.
Akizungumza leo Julai 5, 2025, mkoani Mbeya, Dkt. Madalla alisema changamoto kubwa inayokwamisha maendeleo ya sekta ya mifugo ni uwepo wa magonjwa sugu yanayoshambulia mifugo, hali inayopunguza tija kwa wafugaji na kuathiri ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Serikali imetambua jumla ya magonjwa 11 makuu yanayozuia tija katika sekta ya mifugo. Kwa sasa tumeanza na ugonjwa wa mapafu kwa ng’ombe, lakini pia chanjo dhidi ya ugonjwa wa sotoka kwa mbuzi na kondoo, pamoja na magonjwa ya kuku kama kideli na ndui, zinaendelea,” alisema Dkt. Madalla.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa kugharamia kikamilifu chanjo kwa kuku. Hii ni ishara ya jinsi anavyothamini jitihada za wananchi, hasa wanawake na vijana katika kufuga kuku kwa maendeleo ya familia na taifa,” aliongeza.
Kampeni hii ni muendelezo wa uzinduzi uliofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 16 Juni 2025, katika mji wa Bariadi, Mkoa wa Simiyu, ambapo alizindua rasmi mpango wa kitaifa wa uchanjaji wa mifugo kote nchini.
Kuhusu gharama za chanjo, Dkt. Madalla alisema Serikali imegharamia sehemu kubwa ya gharama ili kuwawezesha wafugaji wengi zaidi kushiriki zoezi hilo. Kwa upande wa ng’ombe, mfugaji atalipia shilingi 500 tu kwa kila mnyama, huku gharama halisi ikiwa ni shilingi 1,000, ambapo Serikali inabeba gharama za usafirishaji, uchanjaji na nusu ya bei ya chanjo.
Kwa mbuzi na kondoo, mfugaji atalipia shilingi 300 kwa kila mnyama, badala ya shilingi 600, na kwa kuku, chanjo ni bure kabisa kwa maelekezo ya Rais Samia, kutokana na umuhimu wa kuku kama chanzo kikuu cha kipato kwa Watanzania wengi, wakiwemo wanawake na vijana.
Akizungumza kwa niaba ya Mkoa wa Mbeya, Adam Mhagama, Kaimu Mratibu wa Chanjo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, alisema mkoa una jumla ya mifugo milioni 3.3, ikijumuisha mbuzi, kondoo, kuku, ng’ombe na wanyama wengine.
“Mpaka sasa, mkoa umepokea chanjo zote ambazo Mhe. Rais alipanga kuzipa Mkoa wa Mbeya, pamoja na vitendea kazi muhimu kama sindano, heleni na kishikwambi kitakachosaidia katika utambuzi wa mifugo kwa njia ya kidijitali kupitia wataalamu wa ngazi ya mkoa na halmashauri,” alisema Mhagama.
“Nitumie nafasi hii kuhamasisha wafugaji wote wa Mkoa wa Mbeya kujitokeza kwa wingi kuchanja mifugo yao na kuhakikisha wanajiandikisha kwa ajili ya usajili wa mifugo ili kupata matokeo bora katika zoezi hili. Chanjo hizi ni muhimu sana katika kudhibiti magonjwa mbalimbali yanayoathiri mifugo yetu,” aliongeza.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbarali, Bi. Oliva Sulle, alisema kuwa wilaya hiyo imepokea zoezi hili kwa mikono miwili na ipo tayari kulisimamia kikamilifu ili liweze kufanyika kwa ufanisi, na kuhakikisha mifugo yote wilayani Mbarali inapata chanjo kwa wakati.
Aliongeza kuwa zoezi la chanjo linaambatana na zoezi la utambuzi wa mifugo, jambo litakalosaidia kuepusha migogoro wilayani Mbarali na kutambua wamiliki wa mifugo mmoja mmoja, hivyo kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika usimamizi wa mifugo.
Akizungumza kwa niaba ya wafugaji wa Kijiji cha Matebete, Wilaya ya Mbarali, Joycelenge Taikoo, alisema wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwapatia chanjo za mifugo ambazo wamekuwa wakizihitaji kwa muda mrefu.
“Chanjo hizi zitasaidia sana kulinda mifugo yetu dhidi ya magonjwa hatari ambayo yamekuwa yakiwadhuru na kuathiri maisha yetu ya kila siku,” alisema Bi. Taikoo.
“Tunahamasishwa na kuwatakia mafanikio katika zoezi hili la uchanjaji na tunaahidi kushirikiana kwa dhati kuhakikisha mifugo yetu inapata chanjo kwa wakati,” aliongeza.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeeleza kuwa imejipanga kuhakikisha kampeni hii ya kitaifa inatekelezwa kikamilifu na kwa mafanikio makubwa katika mikoa yote, ili kuwezesha Tanzania kufungua masoko ya kimataifa kupitia diplomasia ya uchumi na kupunguza utegemezi wa bidhaa za mifugo kutoka nje ya nchi.