SERIKALI YAJADILI NAMNA BORA YA KUMLINDA NA KUMTHAMINI PUNDA
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Nchini, Dkt. Benezeth Lutege, leo Septemba 23, 2026 ameongoza kikao cha wataalamu wa mifugo kutoka Shirika la INADES na ASPA kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mtumba jijini Dodoma.
Kikao hicho kilijikita katika kujadili namna bora ya kumlinda na kumthamini mnyama kazi Punda, pamoja na kuweka mikakati ya kuhakikisha anajumuishwa rasmi katika shughuli mbalimbali za Serikali zinazohusu mifugo, kama ilivyo kwa wanyama wengine.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na umuhimu wa kuwahusisha Punda katika zoezi la chanjo, utambuzi na usimamizi wa mifugo, hatua inayolenga kuimarisha ulinzi na ustawi wa wanyama hao nchini.
Aidha, kikao hicho kilijadili suala la kumuondoa Punda katika kundi la wanyama wanaoliwa, likihusishwa na maazimio ya Wakuu wa Nchi mbalimbali yaliyofikiwa Februari 8, 2024, jijini Dar es Salaam, kuhusu kusitisha biashara ya uchinjaji wa Punda kwa kipindi cha miaka 15.
Hatua hizo zinaelezwa kuwa sehemu ya jitihada za kuimarisha ulinzi, ustawi na matumizi endelevu ya Punda, ambaye amekuwa akitumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii nchini.