SERIKALI YAIDHINISHA USAMBAZWAJI WA HERENI ZA KIELEKTRONIKI KWA WAFUGAJI NCHINI
SERIKALI YAIDHINISHA USAMBAZWAJI WA HERENI ZA KIELEKTRONIKI KWA WAFUGAJI NCHINI
Imewekwa: 12 May, 2025

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesaini mkataba unaoidhinisha usambazwaji wa hereni za kieletroniki zitakazotumika kwenye utambuzi wa Mifugo nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo fupi iliyofanyika kwenye Ofisi za Wizara hiyo jijini Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amewataka wasambazaji hao kuhakikisha taarifa zilizopo kwenye hereni hizo zinakuwa msaada kwa mfugaji pindi anapohitaji kufahamu lolote kuhusu Mifugo yake.
“Muwe tayari wakati wote kutoa elimu kwa wafugaji juu ya namna hereni hizo zinavyofanya kazi ili kuwawezesha wafugaji uelewa wa kutosha kuhusu vifaa hivyo,Amesema Prof. Shemdoe.
Aidha Prof. Shemdoe amebainisha kuwa wafugaji hawatatozwa gharama yoyote wakati wa zoezi la uwekaji hereni hizo baada ya Serikali kugharamia zoezi hilo.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Mifugo Ndg. Abdul Mhinte amewataka wazabuni hao kuhamasisha wafugaji kuweka hereni kwenye mifugo yao ili uwe utamaduni kwa wafugaji hao kufanya hivyo hata kusipokuwa na msukumo kutoka Serikalini.
Kwa upande wa wazabuni hao wameihakikishia Wizara kuzalisha na kusambaza hereni zenye viwango na sifa stahiki ili ziweze kuwasaidia wafugaji wakati wowote wanapohitaji kupata taarifa za Mifugo yao.