Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

SERIKALI YAFUNGUA ZIWA IKIMBA KWA MAFANIKIO

Imewekwa: 13 September, 2025
SERIKALI YAFUNGUA ZIWA IKIMBA KWA MAFANIKIO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imelifungua ziwa Ikimba lililopo mkoani Kagera ikiwa ni miezi 6 tangu ilipolifunga kwa lengo la kuongeza kiwango cha samaki kwenye ziwa hilo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kufungua hafla hiyo Mkuu wa wilaya ya Bukoba Mhe. Erasto Sima ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Kagera Mhe. Fatma Mwasa amewataka wananchi wanaonufaika na uvuvi wa ziwa hilo kutoacha shughuli walizokuwa wakizifanya wakati wote wa ufungaji wa ziwa ili kuwa na uchumi jumuishi kwenye eneo hilo.

“Niwapongeze sana kwa kutii makubaliano ya kutofanya shughuli za Uvuvi katika kipindi chote cha ufungaji wa ziwa na leo sote tumeshuhudia matunda ya uvumilivu wenu” Amesema Mhe. Sima.

Aidha Mhe. Sima amesema kuwa ufunguzi wa ziwa hilo utaongeza mapato ya halmashauri ambapo mpaka sasa takribani shilingi Mil.8 zimeshapatikana kupitia usajili wa mitumbwi ya kuvulia samaki pekee.

“Lakini pia ni muhimu tujiwekee mazoea ya kufunga ziwa angalau kwa miezi 6 ili kuendelea kunufaika na rasilimali za uvuvi zinazotokana na ziwa letu na kuendelea kukuza uchumi wetu” Ameongeza Mhe. Sima.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede amesema kuwa Wizara yake itaendelea kuchagiza shughuli za Uvuvi kwenye ziwa hilo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya Uvuvi unaokubalika kisheria na kuongeza takribani vifaranga Mil.1 vya samaki kabla ya mwisho wa mwezi Oktoba mwaka huu.

“Wataalam wetu wa Wizara wataweka kambi hapa  kwa ajili ya kutoa elimu hiyo lakini pia  watakaa na nyie darasani kabisa ilo kuelimishana kuhusu uvuvi unaofaa” Amesema Dkt. Mhede.

Akielezea hali ya upatikanaji wa samaki ilivyo hivi sasa kwenye ziwa hilo, Mkurugenzi wa Uvuvi nchini Prof. Mohammed Sheikh amesema kuwa kwa mujibu wa utafiti wa kitaalam uliofanyika leo ziwani hapo, kiwango cha Mavuno ya samaki kwa mwaka kinatarajia kupanda kutoka tani 1.5 hadi kufikia tani 15 huku kiwango hicho kikitarajiwa kuongezeka zaidi endapo rasilimali za Uvuvi zilizowekwa ziwani humo zitalindwa kikamilifu.

“Huu ni mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba uzalishaji unaongezeka, wananchi wanapata tija na mapato ya Serikali kupitia sekta ya Uvuvi yanaongezeka” Amesema Prof. Sheikh.

Kwa upande wao Wavuvi wanaonufaika na Ziwa hilo Bw. Benickson Charles na Bi. Rehema Hamza  wamesema kuwa kufunguliwa kwa ziwa hilo na kiwango cha samaki wanaopatikana ni fursa ya wao kukuza uchumi wao kupitia maji hayo ambapo wameongeza kuwa watahakikisha wanalinda rasilimalo hizo ili zisitoweke tena kama ilivyokuwa awali.

Ziwa hilo lilifungwa Machi 12,2025 kwa makubaliano ya hiyari baina ya Serikali, wavuvi na wananchi wanaonufaika na ziwa hilo kwa lengo la kuongeza kiwango cha uzalishaji wa samaki ili kukuza uchumi wa buluuu kwa wakazi wa eneo hilo, mkoa wa Kagera na Taifa kwa ujumla.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo