SERIKALI YAANZA KUTEKELEZA CHANJO YA MIFUGO MKOA WA DAR ES SALAAM

Serikali imeanza kutekeleza Kampeni ya Chanjo ya Mifugo na Utambuzi Kitaifa kwa kuweka ruzuku ya asilimia 100 kwa chanjo za kuku ambazo zitatolewa bila malipo, asilimia 50 kwa chanjo za Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo ili kutokomeza magonjwa matano ya kipaumbele ya mifugo na kuimarisha biashara ya Mifugo na mazao yake.
Akizindua Kampeni hiyo kwa mkoa wa Dar es Salaam leo 3 Julai, 2025 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agness Meena amesema mpango huo wa uchanjaji na Utambuzi wa Mifugo Kitaifa unaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2024-2025 ambapo shilingi bilioni 69.2 zimetengwa na serikali kwa ajili ya kufanikisha Kampeni hiyo nchini.
" Tumeanza Kampeni yetu ya Chanjo na kwa ukanda wa huu wa Pwani tumeanza na Dar es Salaam katika shamba la mfugaji wetu la Zoo hapa Kigamboni, ambapo Zaidi ya Mifugo 200 inachanjwa leo , Serikali itagharamia shilingi 500 na mfugaji kuchangia shilingi 500 kwa chanjo ya ngo’mbe , shilingi 300 kwa chanjo ya mbuzi na Kondoo na mfugaji kuchangia shilingi 300 na chanjo ya kuku itatolewa bure" alisema Bi. Meena.
Aidha, Bi. Meena amesisitiza kuwa katika kutekeleza mpango huu wa chanjo serikali imelenga kukabiliana na magonjwa Matano ya kipaumbele (Priority
Diseases) ili kuyadhibiti na kuyatokomeza nchini na kuwezesha kufungua masoko ya ndani ya Afrika na Nje ikiwepo soko la Ulaya.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni Bw. Kalila Kingi amesema Kampeni ya Chanjo itasaidia kuimarisha biashara ya mifugo na mazao yake katika Manispaa hiyo na kutoa rai kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalam wa mifugo wakati wa utekelezaji wa kampeni hiyo.
Zoezi la uchanjaji litaenda sambamba na Utambuzi na Usajili wa Mifugo kwa uvishaji wa hereni za kieletroniki kwa Wanyama wote watakaochanjwa isipokuwa kuku.