SERIKALI YA AWAMU YA SITA YADHAMIRIA KUIMARISHA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga vyema kuimarisha sekta za mifugo na uvuvi ili kuongeza uzalishaji na kutoa fursa kwa Vijana na wadau wote ili kukuza kipato chao na kipato cha Taifa kiujumla.
Akizungumza wakati wa kuhutubia na kufungua rasmi Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye mkutano wa kwanza kikao cha nne cha Bunge hilo, jijini Dodoma )14.11.2025), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema mikakati ya kukuza sekta ya mifugo katika muhula wa pili wa serikali ya awamu ya sita ni pamoja na kuongeza eneo lililopimwa la shughuli za ufugaji kutoka ekari milioni 3.46 hadi ekari milioni 6 ili kuepusha migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, pamoja na kuongeza wigo wa uzalishaji wa malisho ya mifugo ili kuelekea kwenye ufugaji wa kisasa.
"katika hatua ya kufungua masoko ya kimataifa, serikali itaendeleza chanjo pamoja na utambuzi wa mifugo nchini ili kuongeza ubora wa mazao ya mifugo na kuingia katika kumbukumbu za dunia na kutambulika sokoni." amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
Aidha, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaendelea kuboresha kosaafu ya mifugo, kujenga mabwawa ya kunyweshea mifugo, majosho, machinjio na miundombinu mingine muhimu kwa ajili ya ufugaji, ikiwa na lengo la kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya mifugo na kufungua masoko ya nje ili wafugaji watoke kumtazama ng'ombe na mlio wake bali kwa kutazama uzito wa nyama, ladha, wingi wa maziwa, ubora wa ngozi, kwato na pembe za ng'ombe, ambayo ndiyo itakayoleta mapinduzi ya sekta ya mifugo.
Vilevile, Mhe. Dkt. Samia amebainisha kuwa katika sekta ya uvuvi serikali itaendelea kuelekaza manufaa ya uvuvi wa bahari kuu na kwenye maziwa makuu kwa kukamilisha mradi wa bandari kuu ya uvuvi ya Kilwa Masoko iliyopo mkoani Lindi ambayo itazalisha fursa ya ajira takriban 30,000 na kujenga bandari nyingine Bagamoyo mkoani Pwani, ambayo itafunganishwa na kongani ya viwanda vya samaki.
Pia, ameweka wazi kuwa serikali ya awamu ya sita itafanya mapitio ya leseni za uvuvi kwa lengo la kuifanya nchi na wavuvi waweze kufaidika ipasavyo na fursa za uvuvi wa bahari kuu, pamoja na kutoa mikopo ya boti, dhana za uvuvi, makasha ya kuifadhi samaki na miundombinu ya kukaushia bidhaa hizo.
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kukuza sekta ya uvuvi kwa kuwekeza zaidi kwenye ufugaji kwa njia ya vizimba na mabwawa ya kufugia samaki ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kuongeza kipato na kujikwamua kiuchumi.