SERIKALI, WADAU KUJA NA MPANGO MKAKATI WA UJUMUISHWAJI BIOANUWAI KATIKA UVUVI

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa rai kwa washirika wa maendeleo ya uvuvi wa kitaifa na kimataifa kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii wanazotoka kwa kuendeleza ushirikiano wa kukuza uchumi wa buluu wa Tanzania kupitia ujumuishwaji wa masuala ya bioanuwai katika uvuvi.
Akifunga warsha ya ujumuishaji Masuala ya Bioanuwai katika Usimamizi wa Uvuvi Oktoba 8, 2025 katika Hoteli ya Giraffe Jijini Dar es Salaam, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Dk. Charles Mhina amesisitiza umuhimu wa kujenga uelewa wa pamoja wa kuoanisha uhifadhi wa bioanuwai na vipaumbele vya kitaifa, hasa katika nyanja za usalama wa chakula, maendeleo ya kiuchumi, na ustawi wa jamii.
Dkt. Mhina amefafanua kwamba mafanikio ya muda mrefu ya sekta ya uvuvi yanategemea uhifadhi wa mazingira ya majini na hivyo ni vema masuala yote yaliyomo katika Mfumo wa Kimataifa wa Kunming–Montreal wa Bioanuwai pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Bioanuwai (NBSAP 2025–2030) yakaingizwa katika sera na mifumo ya kitaifa na ya mitaala ya usimamizi wa uvuvi.
“Kila mmoja akienda kuwekeza nguvu katika haya tuliyoyabainisha hapa nina hakika yataenda kuleta mabadiliko katika jamii zetu , kwahiyo washirika wa maendeleo wa kitaifa na kimataifa tukawe mabalozi katika jamii zetu ili kuongeza uelewa wa uhifadhi wa bioanuwai kwa ajili ya kuwainua wavuvi wadogo” alisema Dkt. Mhina.
Aidha, aliwashukuru wadau wote waliowezesha warsha hiyo wakiwemo FAO kwa msaada wao wa kitaalamu na kifedha, washirika wa maendeleo, taasisi za elimu ya juu, na jamii za wavuvi waliotoa mchango mkubwa katika mjadala wa sera na mbinu za utekelezaji.
Akiwasilisha rasimu ya mpango kazi huo Afisa Uvuvi Mkuu ambaye pia ndio mratibu wa SSF Guidelines Dkt.Lilian Ibengwe amefafanua mapendekezo ya rasimu ya mpango kazi huo kwa kuanisha malengo yaliyopendekezwa na timu ya wataalam, watafiti na wadau wa uvuvi ambavyo vitazingatiwa wakati wa ujumuishajumasuala ya bioanuwani katika uvuvi.
Kwa upande wake mdau wa uvuvi ambaye ni Katibu wa Mtandao wa Wanawake Wavuvi na Wachakataji wa Mazao ya Uvuvi Tanzania (TAWFA) Bi. Hadija Malibiche ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na FAO kwa kuja na majadiliano ya pamoja yanayolenga kuboresha ustawi wa viumbe maji kwa ajili ya manufaa ya wavuvi nchini.
Wadau wa maendeleo walioshiriki kufanya mapitio ya rasimu pendekezwa ya mpango kazi huo ni pamoja na IUCN, GIZ, Benki ya Dunia, Jumuiya ya Ulaya na Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) ambao kwa pamoja wametoa ushauri na mapendekezo kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango huo.