SERIKALI, NMB KUSHIRIKIANA KUKUZA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema itaendeleza ushirikiano na benki ya NMB kutekeleza vipaumbele vya sekta ya mifugo na uvuvi vya mwaka 2025/2026 ili kufanya mageuzi ya kiuchumi nchini.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena leo Septemba 26.2025 mara baada ya kukutana ofisini kwa kwake, Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, na kufanya mazungumzo yenye lengo la kuutambulisha uongozi wa benki hiyo na kuwasilisha mikakati iliyowekwa NMB kwa ajili ya kuchangia ukuaji wa sekta ya mifugo na uvuvi.
"Niwahakikishieni ushirikiano mkubwa nyie benki ya NMB kufanya kazi katika shughuli za sekta ya mifugo na uvuvi", amesema Bi. Meena
Katika mazungumzo hayo Bi. Meena amejadiliana maeneo ya kushirikiana kati ya benki hiyo na wizara na kutaja vipaumbele vinne vya wizara kuwa ni kukuza uzalishaji, uuzaji na uongezaji wa mnyororo wa thamani wa mazao ya mifugo na uvuvi, kuimarisha ulinzi na usimamizi endelevu wa rsilimali za sekta ya mifugo na uvuvi, kukuza uwekezaji katika sekta ya mifugo na uvuvi na kuimarisha utafiti, mafunzo na huduma za ugani.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Huduma za Serikali kutoka benki ya NMB Bi. Vicky Bishubo, amempongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuteuliwa na kufanya kazi kwa bidii katika sekta ya Mifugo na Uvuvi.
Bi. Bishubo ametaja na kuainisha mafanikio na shughuli zinazofanywa na benki hiyo kwenye maeneo mbalimbali kama minada ya mifugo, vikundi vya ushirika vya wafugaji ambapo kupitia shughuli hizo za benki wafugaji wamekuwa wakiitumia kutekeleza shughuli za kisekta kwa manufaa ya nchi.