SERIKALI IMEWATAKA WAVUVI KUSALIMISHA ZANA HARAMU ZA UVUVI
SERIKALI IMEWATAKA WAVUVI KUSALIMISHA ZANA HARAMU ZA UVUVI
Imewekwa: 14 May, 2025

Serikali, kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), imewataka wavuvi wote nchini, ambao si waaminifu, kusalimisha zana zao za uvuvi haramu kwa hiari yao wenyewe badala ya kusubiri kufuatwa huko walikojificha na kufanya vitendo vya uvuvi haramu.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede wakati akizungumza na baadhi ya wavuvi na wadau wa uvuvi wa Ziwa Tanganyika katika ziara yake ya kufuatilia shughuli za doria zinavyofanyika na kujua maendeleo na changamoto wanazokutana nazo watumishi wa Serikali katika kufanya doria kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika, leo Mei 14, 2025, katika Kijiji cha Kipili, Wilayani Nkasi, Mkoani Rukwa.
“Ninyi wenyewe wananchi na wavuvi mmesema kwa vinywa vyenu kuwa kuna wavuvi bado wameficha zana haramu za uvuvi majumbani na sehemu mbalimbali, sasa ninawaambia kuwa hizo zana haramu za uvuvi mzisalimishe katika Mamlaka husika ili tuondokane na adha zitokanazo na uvuvi haramu na pia tuwe na uhakika wa uendelevu wa Ziwa letu," amesema Dkt. Mhede.
Vilevile, Dkt. Mhede amewataka wavuvi kuwaambia wavuvi wenzao kuwa wasisubiri kufuatwa na Mamlaka husika maana watafuatwa katika msako unaoendelea na hatimae Sheria itafuata mkondo wake dhidi ya watakaobainika.
Aidha, Dkt. Mhede amewataka na kuwasihi wavuvi wa Ziwa Tanganyika kutofanya uvuvi haramu sio kwa vitendo tu bali pia kwa kufichiana siri, na watoe taarifa kwenye Mamlaka husika ili hatua zichukuliwe kwa baadhi ya wavuvi au mawakala wa wavuvi wasio waaminifu.
Halikadhalika, Dkt. Mhede amewataka Maafisa Uvuvi kutenda kazi zao kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa kisheria ambapo ameelekeza kuwa kutoza ushuru wa mazao ya uvuvi yaliyovunwa kwa njia haramu (mfano samaki wachanga) nalo ni kosa. Amesisitiza kwamba Serikali inatilia mkazo katika kutoza maduhuli kwa mazao ya uvuvi yaliyovunwa kihalali na sio yaliyovunwa kwa njia haramu.
Naye, Mvuvi wa Ziwa Tanganyika, Bw. Juma Yahya, aliongea kwa niaba ya wavuvi wenzake, na kuishukuru Serikali ya awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa hatua walizozichukua katika kudhibiti na kuhakikisha zana za Uvuvi haramu katika Ziwa Tanganyika zinatokomezwa.
Bw. Yahya, ameiomba Serikali kupitia Wizai ya Mifugo na Uvuvi kuongeza Doria ili kuweka Usalama wa mazao ya Uvuvi na wavuvi wenyewe.