Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

SERIKALI IMELENGA KUIINUA SEKTA YA MAZIWA NCHINI - DKT. MHEDE

Imewekwa: 13 September, 2025
SERIKALI IMELENGA KUIINUA SEKTA YA MAZIWA NCHINI - DKT. MHEDE

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imelenga kuiinua sekta ya maziwa nchini kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo mafunzo ya uongezaji thamani yanayotolewa kwa wafugaji nchini ili  sekta hiyo ya maziwa iweze kuongeza mchango  katika pato la Taifa na kuinua uchumi wa wafugaji.

Akizungumza leo Septemba 9, 2025 wakati akifunga mafunzo ya mradi wa Maziwa Faida kwa wafugaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza unaolenga ufugaji wa ng'ombe wa maziwa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede amewataka watekelezaji wa mradi huo ikiwemo LITA na TALIRI  kwa kushirikiana na wadau kuhakikisha inawafikia wanufaika wote wa mradi huo kwa kuendelea kutoa mafunzo mbalimbali yakuongeza thamani ya sekta ya mifugo.

"Maelekezo ya serikali hata dhamira zetu, asikosekane  hata mfugaji mmoja kuifikia idadi ya wafugaji 3,000 ili kuhakikisha malengo ya mradi wetu yanafikiwa kama ilivyokusudiwa na serikali yetu, kwahiyo mafunzo haya yawe endelevu."

Pamoja na maelekezo hayo Dkt. Mhede amewahimiza wafugaji na wananchi kwa ujumla kunywa maziwa angalau nusu lita kwa siku  kwa ajili ya kuimarisha usalama wa chakula na kuwaagiza watekelezaji wa mradi wa Maziwa Faida kuzishirikisha taasisi za fedha na bima ili zitoe elimu ya kuongeza thamani ya mifugo kwa kufanya ufugaji endelevu wenye tija.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo Dkt. Pius Mwambene  amesema ni wakati sasa wafugaji kuwa tayari kubadilisha mifumo ya ufugaji ili kuendana na ufugaji utakaongeza uzalishaji wa mazao ya mifugo ili kuvihudumia viwanda hapa nchini na kuazalija ajira kwa wananchi.

Naye Mratibu Mkuu wa mradi wa Maziwa Faida Dkt. Zabron Nziku amesema mradi huo  umefadhiliwa na serikali ya Ireland na unatekelezwa na Mamlaka ya Utafiti Ireland (TEAGASC), Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania  (TALIRI) na Wakala ya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) ambapo  unagharimu Shilingi Bilioni 7 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia  2021/2022 hadi 2025/2026 na  kufikia Mwezi Juni mwaka huu jumla  wafugaji  2,239  wamefikiwa na  mradi huku lengo ni kuwafikia wafugaji 3,000.

Aidha, Kiwango cha unywaji wa maziwa kimeongezeka kutoka wastani wa lita 67.5 Mwaka 2023/2024 hadi lita 68.1 Mwaka 2024/2025.

Hata hivyo Wizara imeendelea kuimarisha biashara ya maziwa ambapo mwaka 2024/2025 jumla ya lita za maziwa 90,416,788.5 zenye thamani ya shilingi bilioni 226 zilisindikwa na kuuzwa katika masoko ya ndani ya nchi.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo