RAS ARUSHA ASISITIZA KUENDELEA KUFANYIKA TAFITI ZA MIFUGO NA UVUVI

Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha Bw. Missaile Musa amewataka wataalam wa sekta za Mifugo na Uvuvi kuendelea kufanya tafiti mbalimbali zinazolenga kupata suluhu za changamoto zinazowakabili wafugaji na wavuvi nchini.
Bw. Musa amebainisha hayo wakati akifunga Kongamano la 48 la kisayansi la chama cha wanasayansi ya uzalishaji kwenye sekta za Mifugo na Uvuvi (TSAP) Septemba 26 jijini Arusha ambapo amewataka wataalam hao kuhakikisha wanatafsiri kwa vitendo tafiti walizozifanya kwa mwaka huu.
“Sekta hizi ni muhimu sana kwa sababu kwenye ule mnyororo wake wa thamani watu wengi wamenufaika hivyo tafiti zenu ni tija kwa nchi na uchumi unakuwa kutokana na tafiti hizo” Amesema Bw. Missaile.
Awali akimkaribisha Mgeni rasmi, Mwenyekiti wa chama hicho aliyemaliza muda wake Dkt. Jonas Kizima amesema kuwa mbali na mijadala yenye tija iliyofanyika wakati wote wa kongamano hilo, wanasayansi hao pia walipata fursa ya kufanya utalii wa ndani kwa kupanda mlima Kilimanjaro huku wengine wakitembelea viwanda vya kusindika maziwa na nyama pamoja na shamba la Mifugo.
Nao baadhi ya washiriki wa kongamano hilo Bw. Hamis Mohammed na Bi. Asha Churu wameeleza kuwa watatumia vema fursa waliyoipata kitaaluma kupitia jukwaa hilo kwenda kuboresha shughuli za Ufugaji na Uvuvi pindi watakaporejea kwenye maeneo yao.
Kongamano hilo pia liliambatana na uchaguzi mkuu wa chama hicho ambapo Bw. Zabron Nziku amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Chama hicho akichukua nafasi ya Dkt. Jonas Kizima ambaye amemaliza muda wake.