RAI YATOLEWA KWA WAFUGAJI KWA VIZIMBA KUSHIKWA MKONO ZAIDI

Imewekwa: Friday 21, March 2025

RAI YATOLEWA KWA WAFUGAJI KWA VIZIMBA KUSHIKWA MKONO ZAIDI

Serikali imetoa wito kwa wawekezaji na watoa huduma mbalimbali zikiwemo taasisi za kifedha kuuangana na serikali pamoja na sekta binafsi ili kuwezesha wawekezaji wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba waendelee kufanya vizuri zaidi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede amebainisha hayo Machi 20, 2025 wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Musoma mkoani Mara, kushuhudia maendeleo ya uwekezaji wa vizimba katika ukanda wa mkoa huo.

Akishuhudia uvunaji wa samaki aina ya sato wanaofungwa kwa njia ya vizimba kwenye Ziwa Victoria kupitia uwekezaji wa Kampuni ya GODWIN LUSASO General Supply ltd, Dkt. Mhede ametoa rai kwa wananchi kuwa na utaratibu wa kukusanya fedha kidogo kidogo na kuzihifadhi kwa kuwa mwekezaji huyo ametumia fedha zake mwenyewe na kwamba serikali itaendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu ili Sekta ya Uvuvi ikue zaidi.

Amefafanua kuwa mwekezaji huyo alianza na vizimba vitatu lakini hadi sasa ana vizimba 18 ambapo awamu hii ya kwanza anavuna kwenye vizimba sita na anachovuna kwa sasa kinalipa gharama za uwekezaji wote alioweka ikiashiria wazi namna biashara hiyo inavyolipa na kubainisha samaki hao ni bora.

“Tumekuja na wenzetu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na Maabara ya Taifa ya Uvuvi (NFQCLAB) ambao kazi yao ni kufanya mapitio ya ubora wa samaki wanaovunwa hapa, ninawatoa wasiwasi watanzania hawa samaki hawana matatizo ya kimaabara ni bidhaa bora.” Amesema Dkt. Mhede

Ameongeza kuwa wawekezaji wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba wataunganishwa katika masoko mbalimbali vikiwemo viwanda vya kuchakata samaki hivyo ni muhimu kuwepo na ushirikiano wa pamoja kati ya viwanda na wawekezaji ili kuwa na masoko ya uhakika.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma Bw. Juma Chikoka, amesema upande wa Musoma fursa ya uwekezaji kwa njia ya vizimba ipo kwa sababu eneo kubwa la Wilaya ya Musoma limezungukwa na utajiri wa Ziwa Victoria.

Bw. Chikoka ametoa wito kwa wananchi, wafanyabiashara, wawekezaji na maeneo mengine nchini kuja kuwekeza ufugaji wa kisasa kwa njia ya vizimba kwa kuwa matokeo yake ni makubwa na hii inajenga fursa nyingine ya ajira na uchumi wa Manispaa ya Musoma na Musoma vijijini.

Aidha, amesema mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuwekeza katika ufugaji wa kisasa kwa njia ya vizimba hususan katika mkakati wa Uchumi wa Buluu.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya GODWIN LUSASO General Supply ltd Bw. Godwin Kababaye amebainisha kuwa katika uwekezaji wake kwenye ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba awamu hii ya kwanza anavuna takriban tani 50 ambapo anachukua uwekezaji huo kama fursa kwake na ajira kwa wengine.

Bw. Kababaye ameongeza kuwa katika uwekezaji wake ametumia zaidi ya Shilingi Milioni 430 lakini anahitaji nguvu zaidi kwa kuwa matamanio yake ni kujenga kiwanda cha kuchakata samaki na kuiomba serikali kuweka nguvu zaidi katika upatikanaji wa chakula cha kutosha cha samaki na idadi kubwa ya vifaranga ya samaki na vyenye ubora ili wafugaji wa samaki waweze kufuga samaki wengi zaidi.

Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede alipata fursa ya kutembelea vizimba vya mradi unaofadhiliwa na serikali kwa vikundi vidogo na kujionea maendeleo ya mradi huo.


*Mwisho* .

.