Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

PWANI KUCHANJA NA KUTAMBUA MIFUGO YOTE KWA SIKU 30

Imewekwa: 21 July, 2025
PWANI KUCHANJA NA KUTAMBUA MIFUGO YOTE KWA SIKU 30

Uongozi wa mkoa wa Pwani umesema kuwa utatumia siku 30 pekee kuchanja na kutambuaMifugo yake badala ya miezi 2 iliyopangwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutekeleza zoezi hilo.

Ahadi hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Shaib Ndemanga ambaye pia alimwakilisha mkuu wa Mkoa huo kwenye ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji iliyolenga kukagua Utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo kwenye kwenye kijiji cha Miono Wilaya ya Chalinze.

“Tunajua nyie kama Wizara mmepanga kutekeleza awamu ya kwanza ya zoezi hili kwa miezi miwili lakini nikuhakikishie Mhe. Waziri mkoa wa Pwani kwa furaha tuliyonayo na namna tulivyopokea zoezi hili tutahakikisha tunamaliza ndani ya siku 30” Amesema Mhe. Ndemanga.

Akizungumza mara baada ya kushuhudia kuanza kwa utekelezaji wa kampeni hiyo mkoani Pwani, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameupongeza mkoa huo kwa namna walivyopokea zoezi hilo alilolitaja kama sehemu ya maono makubwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upande wa sekta ya Mifugo na wafugaji kwa ujumla.

“Tumeshaanza majadiliano na nchi 5 wanaohitaji kuchukua mifugo yetu ikiwa hai na hiyo inamaanisha kwa sasa soko la Mifugo yetu limeonekana na kwa hapa Pwani tuna kiwanda kikubwa cha kusindika nyama ambacho kitaweza kufikia asilimia 100 za uwezo wake tofauti na ilivyo sasa ambapo kinafanya kazi kwa asilimia 50 ya uwezo wake” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji.

Naye Mwenyekiti wa chama cha Wafugaji mkoani humo Bw. Ngobere Msamau mbali na kuishukuru Serikali kutokana na chanjo hizo amemhakikishia Mhe. Dkt. Kijaji kuwa wataendelea kutekeleza ushauri na maelekezo yote wanayopewa na Serikali baada ya tija kubwa waliyoanza kuipata hivi sasa.

Ziara hiyo ya Mhe. Dkt. Kijaji iliyolenga kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo iliyozinduliwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Juni 16, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea katika mkoa wa Morogoro Julai 10, 2025.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo