Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

PROF SHEIKH ATAKA MITAALA YA FETA IENDANE NA MAHITAJI YA DIRA YA MAENDELEO YA TAIFA 2050

Imewekwa: 27 September, 2026
PROF SHEIKH ATAKA MITAALA YA FETA IENDANE NA MAHITAJI YA DIRA YA MAENDELEO YA TAIFA 2050

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Prof. Mohammed Sheikh ametaka Mitaala inayohuishwa na inayopendekezwa kuanzishwa na Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kuendana na mahitaji ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050.

Prof. Sheikh ametoa kauli hiyo 25 Septemba, 2026 alipokuwa anafungua kikao cha kuwasilisha Rasimu ya mitaala iliyohuishwa na inayopendekezwa kuanzishwa na FETA  kwenye Menejimenti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kilichofanyika Mtumba, Dodoma.

Amebainisha kwamba zoezi hili la uhuishaji na uanzishaji wa mitaala mipya ni muhimu kwa wakati huu sababu kuna mabadiliko makubwa ya sera, sayansi, teknolojia na diplomasia ya masoko ya ndani na ya kimataifa, hivyo mitaala lazima iendane na mabadiliko yaliyopo sasa.

Aidha amesema kuwa mabadiliko haya ya mitaala ni lazima yaendane na mafunzo kwa wakufunzi wa FETA hasa kwa kupitia kubadilishana uzoefu na vyuo vingine, hususan vya nje ya nchi ili waweze kuendana na mabadiliko ya teknolojia yaliyopo hivi sasa.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa FETA Dkt. Semvua Mzighani amesema kwamba mitaala hii itakapoanza kutumika itaongeza fursa zipatikanazo toka katika Uchumi wa Buluu na hivyo kuongeza ajira, uhakika wa chakula, uhifadhi wa mazingira na Pato la Taifa kwa ujumla.

Mitaala inayohuishwa na inayopendekezwa kuanzishwa na FETA inajumuisha matumizi ya teknolojia za kisasa kama vile Akili Unde (Artificial Intelligence),  Mtandao wa Vitu (Internet of Things) na ndege nyuki (Drones).

Mrejesho, Malalamiko au Wazo