Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

NIGERIA YAVUTIWA NA MPANGO KABAMBE WA MIFUGO TANZANIA

Imewekwa: 14 May, 2025
NIGERIA YAVUTIWA NA MPANGO KABAMBE WA MIFUGO TANZANIA
Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Mifugo ya nchini Nigeria ikiongozwa na Mkurugenzi Mratibu wa Programu za Kitaifa wa Wizara hiyo, Dkt. Ishiyaku Mohammed imeonesha kuvutiwa na namna Tanzania inavyotekeleza Mpango Kabambe wa Mifugo Tanzania (Tanzania Livestock Master Plan) katika kuboresha sekta ya mifugo. Hayo yamefahamika wakati wa kikao baina ya Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe na timu hiyo ya Wataalamu kutoka nchini na Nigeria kilichofanyika katika ofisi za wizara zilizopo Mji wa Serikali, Mtumba, jijini Dodoma leo Mei 13, 2025. Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Mohammed amesema kuwa lengo la ziara yao ni kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna Tanzania ilivyofanikiwa kutekeleza mpango kabambe huo ili iwasaidia katika kufanya maandalizi ya utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Mifugo wa Nigeria (NLMP) wanaotarajia kuuanzisha. Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe ameieleza timu hiyo kuwa Serikali imeendelea kuimarisha sekta ya mifugo kupitia Mpango Kabambe huo ambao umechangia kuboresha maeneo ya Afya ya Mifugo, Malisho na Maji pamoja na kuzalisha Mbegu Bora. Aidha, Prof. Shemdoe ameongeza kuwa pamoja na mpango huo serikali imeandaa kampeni ya chanjo kwa mifugo inayotarajiwa kuzinduliwa na Rais wa Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itakayo saidia mifugo kuwa na afya bora ili kukidhi vigezo vya soko la kimataifa.
Mrejesho, Malalamiko au Wazo