NI BAJETI YA KISHINDO SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI
NI BAJETI YA KISHINDO SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI
◼️Bunge laidhinisha Shilingi Bil. 433.4 kutumika 2026/2027
◼️Dkt. Bashiru aanika vipaumbele vya bajeti hiyo
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya shilingi Bil.433.4 mara baada ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa kuwasilisha vipaumbele na mikakati ya utekelezaji wa bajeti hiyo kwa mwaka 2026/2027.
Akiainisha vipaumbele hivyo, Balozi Dkt. Bashiru amesema kuwa kipaumbele cha kwanza ni kuongeza uzalishaji, masoko na thamani ya mazao ya mifugo na uvuvi ambapo katika kutekeleza kipaumbele hicho wizara hiyo itaboresha mbari za mifugo na viumbemaji ikiwemo madume, mitamba na vifaranga vya samaki huku pia ikiimarisha upatikanaji wa malisho, mbegu za malisho, vyakula vya mifugo na samaki, na upatikanaji wa maji kwa kuzingatia hifadhi ya mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi.
“Pia Wizara itaimarisha afya ya mifugo na viumbemaji, huduma bora za maabara, mifumo ya utambuzi wa mifugo na mifumo ya kidigitali katika uzalishaji, masoko na biashara ya mazao ya mifugo na uvuvi huku pia tukiimarisha matumizi ya zana, mitambo na teknolojia za kidigiti katika uzalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi na ufuatiliaji wa bidhaa na huduma za ugani kwa kuimarisha ubia na sekta binafsi katika kukuza chapa na uthibitishaji wa bidhaa za mifugo na uvuvi za Tanzania katika masoko ya kimataifa” Amesema Balozi Dkt. Bashiru.
Aidha Balozi Dkt. Bashiru amelieleza Bunge kipaumbele cha pili cha Wizara yake mwaka ujao wa fedha kuwa ni kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za mifugo na uvuvi kwa kufanya mapitio ya sheria, miongozo na kanuni zinazosimamia rasilimali za mifugo na uvuvi, kuanzisha vyombo maalum vya utendaji kwa ajili ya kusimamia na kulinda rasilimali za mifugo na uvuvi, kuboresha vituo vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za mifugo na uvuvi;kurasimisha biashara za mazao ya mifugo na uvuvi ili kudhibiti uuzaji holela na kutenga maeneo muhimu ya hifadhi na mazingira ya bahari na maji mengine.
“Mhe. Spika kipaumbele chetu cha 3 kwa mwaka ujao wa fedha ni kuhamasisha uwekezaji katika Sekta za Mifugo na Uvuvi ambapo miongoni mwa ya utekelezaji wa kipaumbele hiki ni kuimarisha Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) ili kuchagiza na kujenga uwezo wa vijana na wanawake kujiajiri katika shughuli za mifugo, uvuvi na ukuzaji viumbemaji na kuimarisha uwezo wa kuvua samaki katika bahari kuu na maji mengine kwa kuwawezesha wavuvi kupata vifaa vya kisasa vya uvuvi na ukuzaji viumbemaji” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.
Balozi Dkt. Bashiru alihitimisha vipaumbele vinavyotarajiwa kutekelezwa na Wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha kuwa ni kuimarisha utafiti, mafunzo na huduma za ugani kwenye Sekta za Mifugo na Uvuvi kupitia mikakati ya kuboresha huduma za utafiti, mafunzo na ugani kwa wafugaji, wavuvi na wakuzaji viumbemaji,kuimarisha uwezo wa miundombinu na rasilimaliwatu katika taasisi za utafiti na mafunzo ya Mifugo na Uvuvi,kutoa mafunzo yenye ithibati kwa mabaharia wa meli za uvuvi wa bahari kuu, waendeshaji wa vyombo vya uvuvi, waangalizi na wakaguzi wa uvuvi, kuimarisha ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa katika utafiti, mafunzo na huduma za ugani katika Sekta za Mifugo na Uvuvi, kuimarisha uwezo wa taasisi katika kuhaulisha teknolojia za kuongeza uzalishaji katika Sekta za Mifugo na Uvuvi na kuwekeza katika utafiti wa ufanisi wa matumizi ya chakula cha wanyama, udhibiti wa magonjwa na mifumo ya ufugaji inayostahimili mabadiliko ya Tabianchi.