MTENDAJI MKUU WA MAHAKAMA AMTAJA DKT. KIKWETE KWA KUMJENGEA MSINGI

Imewekwa: Wednesday 01, September 2021

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amesema anamshukuru sana Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuwa ndiye aliyemuibua katika uongozi mwaka 2013 kwa kumteua kwa mara ya kwanza kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamadani na Michezo.

Prof. Gabriel amebainisha hayo (30.08.2021) wakati akizungumza na menejimeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika ofisi za wizara hiyo jijini Dodoma, wakati alipofika kwa ajili ya kukabidhi ofisi aliyokuwa akihudumu katika nafasi ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo.

Aidha, Prof. Gabriel amebainisha kuwa siku chache kabla ya Mhe. Dkt. Kikwete kuondoka madarakani Mwezi Oktoba Mwaka 2015, alimteua kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamadani na Michezo hivyo hana budi kumshukuru kwa kuwa alionesha imani kubwa kwake.

Pia, amesema anashukuru aliendelea kuaminiwa na Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alimteua kushika nafasi ya Katibu Mkuu wizara tofauti na Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye alimteua kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo nafasi ambayo alikuwa akiendelea kuihudumu hadi alipomteua tena hivi karibuni kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.

“Namshukuru sana Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na imani nami katika nafasi hii mpya aliyoniteua ya kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, na kwamba nitafanya kazi kwa nguvu na weledi mkubwa kwa kushirikiana na wenzangu kwa kuwa nina deni kubwa la kulipa kwa Mhe. Rais Samia, lakini pia kufikia matarajio ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma na matarajio ya watanzania wote katika mhimili huu kwenye utendaji wa haki.” Amesema Prof. Gabriel

Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amefanya mazungumzo na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), katika ofisi za wizara hiyo ambapo Waziri Ndaki amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na imani kubwa na Prof. Gabriel kwa kumteua kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kutoka katika nafasi aliyokuwa akihudumu ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo.

Waziri Ndaki amesema uteuzi aliopata Prof. Gabriel kusimamia mhimili muhimu katika taifa hili kwenye masuala yanayohusu haki kwa watanzania na kwamba jambo hilo ni kubwa kwa kuwa ni mhimili muhimu kwa taifa.

“Mimi nikupongeze kwa kuaminiwa kwa kiasi hicho, kwa sababu ni kwa kiasi kikubwa kwa kweli lakini nichukue nafasi hii kukushukuru kwa muda ambao tumefanya kazi pamoja.” Amesema Mhe. Ndaki

Mhe. Ndaki amesema wakati Prof. Gabriel alipokuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika sekta ya mifugo amekuwa msaada mkubwa kwake katika utendaji kazi na kwamba amekuwa akitoa maelekezo na usimamizi wa majukumu mbalimbali ya wizara na kutengeneza timu ambayo inaelewa majukumu yake.

Ameongeza kuwa wakati wa uwepo wake katika wizara hiyo Prof. Gabriel amekuwa ni mtu wa kujitolea na kufanya kazi muda wowote bila kujali siku wala saa na kwamba watumishi wengi wa wizara wanaweza kufanya mambo makubwa na wizara itaendelea kuhitaji ushirikiano wake wa karibu kwa ajili ya kupata uzoefu kutoka kwake kwa yale aliyokuwa akisimamia wizarani hapo.

Awali mara baada ya kukabidhiwa nyaraka muhimu za ofisi ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi inayoshughulika na Mifugo, Kaimu Katibu Mkuu Bw. Amosy Zephania amemshukuru Prof. Elisante Ole Gabriel wakati wa utumishi wake wa miaka mitatu katika wizara hiyo kwa kuwa amejenga msingi mkubwa wizarani hapo.

Bw. Zephania amefafanua kuwa atahakikisha anasimamia misingi iliyoachwa na Prof. Gabriel na kuhakikisha anaisimamia vyema sekta ya mifugo ili iendelee kuleta tija kwa wananchi hususan wafugaji na kuzingatia yote ambayo mtendaji mkuu huyo wa mahakama amewaachia yakiwemo ya kushirikiana kwa viongozi na wafanyakazi wote kwa ujumla.

.