MSIWASIKILIZE WAPOTOSHAJI KUHUSU CHANJO YA MIFUGO-MNYETI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti ametoa rai kwa wafugaji nchini kutowasikiliza watu wanaopotosha kuhusu Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo kwani inalenga kuboresha mazingira ya mifugo na biashara kimataifa.
Naibu Waziri Mnyeti amebainisha hayo (04.07.2025) wakati akikagua utekelezaji wa kampeni hiyo katika katika Kijiji cha Nsola kilichopo Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza ambapo amesema utoaji wa chanjo na utambuzi wa mifugo hauna uhusiano wowote na wafugaji kudaiwa mapato.
“Natoa wito kwa wafugaji wote, wale wanaopotosha ukweli kuhusu chanjo za mifugo pamoja na habari ya utambuzi, wengine wanasema eti TRA watakuja kutudai, tunazungumzia habari ya kutambua mifugo yetu ili tupate pia idadi ya mifugo iliyopo nchini.” amesema Mhe. Mnyeti
Ameongeza kuwa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo itaiwezesha serikali kujenga majosho kulingana na idadi ya mifugo iliyopo nchini pamoja na kuweka mazingira mazuri ya mifugo yakiwemo maeneo ya machungio na malisho.
Kupitia kampeni hii serikali imetoa ruzuku ya asilimia 100 kwa kuku ambapo watachanjwa bure huku ng’ombe, mbuzi na kondoo ikitoa ruzuku ya asilimia 50.