Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MIKATABA YA UBORESHAJI KITUO CHA UKUZAJI VIUMBE MAJI KINGOLWIRA YASAINIWA

Imewekwa: 06 September, 2025
MIKATABA YA UBORESHAJI KITUO CHA UKUZAJI VIUMBE MAJI KINGOLWIRA YASAINIWA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena ameongoza zoezi la utiaji saini mikataba baina ya serikali na wakandarasi watakaotekeleza miradi ya ukarabati wa vitotoleshi vya vifaranga vya Samaki, ujezi wa  mifumo ya hewa kwenye mabwawa ya kufugia samaki, uchimbaji wa visima vya maji eneo la Kingolwira mkoani Morogoro na ujenzi wa Soko la Samaki  Kipumbwi katika wilaya ya Pangani mkoa wa Tanga  na kuwataka wakandarasi hao kukamilisha miradi hiyo kwa wakati na kuzingatia viwango vya ubora kama mkataba unavyoelekeza. 

Bi. Meena amesema hayo leo Agosti 29, 2025 katika ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo mji wa serikali Mtumba Jijini Dodoma mara baada ya kusaini mikataba minne na wakandarasi hao ambapo aliwasisitiza kuzingatia muda na ubora wa miradi kulingana na makubaliano ya Mkataba.

" Miradi hii ni ya kimkakati kwa wizara yetu na kama mnavyojua inawagusa moja kwa moja wananchi hivyo mtekeleze  kwa kuzingatia muda na ubora wa mikataba ili uwanufaishe wananchi wetu." Alisema, Bi. Meena.

Kwa upande wao wakandarasi  wa miradi hiyo wameahidi kutekeleza mikataba yao kwa wakati na kuzingatia ubora ili ianze kufanya kazi.

Mikataba iliyosainiwa ni pamoja na Mkataba wa  kuchimba visima viwili vya maji eneo la Kingolwira Mkoani Morogoro unaotekelezwa na Kampuni ya EF. IMER CONSTRUCTION CO. LTD, Mkataba wa ujezi wa mifumo ya hewa Katika Mabwawa ya kufugia samaki  Kingolwira unaotekelezwa na kampuni ya Kanuta Engineering and Supply Limited.

Mikataba mingine ni ile ya ujenzi wa vitotoleshi vya Vifaranga vya samaki Kingolwira Morogoro, unaotekelezwa na Kampuni ya KPM investment LTD na Ujenzi wa Soko la Samaki eneo la Kipumbwi Pangani Tanga ambao unatekelezwa na Kampuni ya WCEC LIMITED kutoka  Dar es salaam.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo