MIFUGO MILIONI 61 KUCHANJWA NA KUFANYIWA UTAMBUZI AWAMU YA PILI
Serikali imelenga kuchanja zaidi ya mifugo milioni 61 katika awamu ya pili ya kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo, huku ikisisitiza utekelezaji wa kampeni hiyo uzingatie magonjwa yanayosumbua maeneo husika ili kuongeza ufanisi na kupunguza hasara kwa wafugaji.
Akifungua kikao cha tathmini ya awamu ya kwanza na maandalizi ya awamu ya pili ya Mpango wa Kampeni ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo Kitaifa, leo Oktoba 13, 2026 Jijini Dodoma, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amesema serikali ya awamu ya sita ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kuendelea kuimarisha na kupanua wigo wa chanjo nchini, na kwa mwaka huu wa fedha inaendelea kutekeleza kampeni hiyo ambayo inalenga kuchanja magonjwa sita muhimu ya mifugo.
“Serikali inalenga kuchanja magonjwa sita muhimu ya mifugo, ambayo ni Mdondo, Ndui na Mafua kwa kuku milioni 40, kadhalika ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo (PPR) wanyama million 9.3, pamoja na Ugonjwa wa Homa ya Mapafu ya Mbuzi (CCPP) mbuzi milioni 3.7, na ng’ombe million 7.9 ambao watachanjwa dhidi ya Ugonjwa wa Mapafu ya Ng'ombe (CBPP)”. Mhe. Balozi Dkt. Bashiru
Aidha, Dkt. Bashiru amewataka wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na watendaji wengine wa serikali wakiwemo Maafisa Mifugo kusimamia kwa ukaribu kampeni hiyo ili kuweza kuleta matokeo tarajiwa, na amewataka wataalamu kuhakikisha wanyama wote ambao hawakutambuliwa wakati wa chanjo ya awamu ya kwanza na wale watakao chanjwa awamu hii watambuliwe kwa kuvalishwa hereni za kielekroniki na taarifa zake kuingizwa kwenye mfumo wa Utambuzi.
Vilevile, Dkt. Bashiru amewaonya wananchi ambao wapotosha umma kupitia mitandao ya Kijamii kwa kurusha taarifa ambazo zinaleta taharuki kwa jamii hususan kuhusu Mifugo na Uvuvi, na amewataka wananchi kuhakiki taarifa wanazopata kutoka Mamlaka husika na sio kupotosha jamii kwani ni kinyume na takwa la sheria, na ameweka bayana kuwa Serikali ina mifumo imara ya kuhakikisha ubora wa mazao ya Mifugo na uvuvi.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Wakuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ambaye ni Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dodoma Jiji, Bw. Gratian Mwesiga ameiomba Wizara kuhakikisha chanjo zinatolewa kwa kuzingatia kalenda ya taifa ya chanjo na taarifa za vituo vya mifugo vya kanda kuhusu magonjwa yanayoathiri maeneo husika, ili aina na huduma za chanjo ziendane na mahitaji halisi ya wafugaji.