Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. MNYETI-UMEKAA NA NG'OMBE ANALINGANA KILO NA WEWE! MCHANJE, MUOSHE NA UMTIBU.

Imewekwa: 06 July, 2025
MHE. MNYETI-UMEKAA NA NG'OMBE ANALINGANA KILO NA WEWE! MCHANJE, MUOSHE NA UMTIBU.

Serikali imesema ili mifugo iwe na thamani pamoja na ubora wa kimataifa ni lazima ichanjwe dhidi ya magonjwa, kuoshwa na kutibiwa kwa ajili ya kuondokana na umasikini wa wafugaji na taifa kwa ujumla.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amebainisha hayo (05.07.2025) katika Kijiji cha Mahembe kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga, wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo, ambapo amesema pamoja na utajiri mkubwa wa wafugaji ni lazima wajue thamani ya mifugo waliyonayo.

“Unakuta ng’ombe amekondeana kama mfugaji sababu hautaki kumtibu umekaa na ng’ombe analingana kilo na wewe.” amesema Mhe. Mnyeti

Aidha, amewakumbuha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapenda sana wafugaji hadi serikali kulazimika kubeba gharama kwa kutenga Shilingi Bilioni 280 kwa ajili ya zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo nchi nzima.

Akisoma taarifa ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika halmashauri hiyo Dkt. Mwita Wariuba, amesema katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 wamepokea chanjo 280,000 ya ng’ombe dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu, chanjo kwa ajili ya mbuzi na kondoo dhidi ya ugonjwa wa sotoka dozi 152,000 na chanjo ya kuku dhidi ya magonjwa ya mafua, ndui na kideli dozi 300,000 pamoja na vifaa vya kutolea chanjo.

Aidha, ameongeza kuwa halmashauri imepokea pia vifaa vya utambuzi wa mifugo zikiwemo hereni za kieletroniki 90,000 kwa ajili ya ng’ombe na hereni 60,000 kwa ajili ya mbuzi pamoja na kifaa kimoja cha kuvishia hereni.

Naye mmoja wa wafugaji wakubwa katika Kijiji cha Mahembe Bw. Masanja Rushu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo kwa kuwa chanjo zimekuwa zikiwasumbua kwa muda mrefu.

Serikali imetoa ruzuku kwa chanjo za mifugo katika kampeni hii ambapo kuku wanachanjwa bure, ng’ombe Shilingi 500 wakati mbuzi na kondoo Shilingi 300.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo