MAZIWA NI UCHUMI, TUCHANGAMKIE FURSA-RC JAMES
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Kheri James amewataka Watanzania kuchangamkia fursa za kiuchumi zitokanazo na maziwa.
Mhe. James amebainisha hayo Juni 01,2026 kwenye kongamano la wadau wa tasnia hiyo wakati akifunga Maadhimisho ya 29 ya wiki ya maziwa yaliyokuwa yakifanyika mkoani Iringa.
“Siku hii ina umuhimu sana kwa sababu kwanza huongeza uelewa kuhusu faida za maziwa kwa watoto, vijana, wazazi na wazee, pili huhamasisha matumizi ya lishe bora kwa jamii, tatu huunga mkono wafugaji na sekta ya mifugo kwa kuongeza matumizi ya maziwa na bidhaa zake na kukuza uchumi kupitia uzalishaji, usindikaji, na ajira zinazotokana na sekta ya maziwa nchini” Amesema Mhe. James.
Aidha Mhe. James amewataka wananchi kutoishia kusherehekea pekee bali watumie siku hiyo kujenga utamaduni wa kunywa maziwa yaliyosindikwa angalau kwa wastani wa glasi moja kwa siku kwa ustawi wa afya zao na maendeleo ya uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Prof. George Msalya amesema kuwa maziwa ni chakula chenye thamani kubwa na pindi mmoja anapoyatumia afya yake huimarika.
“Maziwa ni chakula cha asili kinachoanzisha maisha kwa kila mmoja wetu kwa sababu hakuna mtu ambaye hajawahi kunyonya maziwa na kitaalam virutubisho vilivyopo kwenye makundi yote ya vyakula na vinavyotakiwa kwenye mwili ni 120 na nusu ya virutubisho hivyo ni maziwa” Ameongeza Prof. Msalya.
Kupitia kongamano la wadau wa maziwa liliohitimisha Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Maziwa ambayo kwa mwaka huu wadau wamekubaliana kuhakikisha wanarasimisha maziwa kuanzia ngazi ya mfugaji hadi mlaji.