MAJOKOFU 184 YA KUHIFADHIA CHANJO YA MIFUGO KUSAMBAZWA KWENYE HALMASHAURI 184

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema serikali inaendelea kukamilisha maandalizi ya Kampeni ya Kitaifa ya chanjo na Utambuzi wa mifugo ambapo jumla ya majokofu 184 yatagawiwa katika Halmashauri zote 184 nchini ili kufanikisha zoezi la uchanjaji
Mhe. Dkt. Kijaji amesema hayo Machi 21, 2025 katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo Temeke Jijini Dar Es Salaam wakati akipokea Majokofu 60 ambayo yamelenga kuboresha mnyororo baridi ya Chanjo ya Mifugo nchi nzima kutoka Kampuni ya Hester Bioscience Africa Limited.
Mhe. Dkt. Kijaji alisema Serikali ilisaini mikataba na wazalishaji wa chanjo ambapo kampuni tatu za ndani ikiwemo Hester Bioscience Africa Ltd, Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) na NOVAB ziliingia makubaliano ya kutoa Majokofu kwa ajili ya kuhifahdi chanjo hizo ili zisihalibike.
“Kampuni ya Hester Bioscience Africa Ltd tulikubaliana watupatie majokofu 100 na leo hii wamekabidhi Majokofu 60, tunawasisitiza wakamilishe zote 100, tayari tulishapokea majokofu 40 kutoka kampuni zingine ambazo zimepelekwa Mwanza, " alisema Dkt. Kijaji.
Mhe. Dkt. Kijaji ameongeza kusema kuwa serikali itaendelea kukamilisha maandalizi ya zoezi la Chanjo na utambuzi wa Mifugo kitaifa kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameridhia bajeti ya Shilingi Billioni 28 zitumike kwaajili ya chanjo ya mifugo kwa mwaka wa fedha 2024/ 2025 huku mpango huo ukitarajiwa kufanyika kwa kipindi cha miaka mitano.
Kwa upande wake Mwekezaji wa kampuni ya Hester Bioscience Africa Ltd Bw. Rajiv Gandhi alisema kuwa ni heshima kubwa kwa kampuni yake kuwepo kwenye mpango wa Taifa wa uchanjaji pamoja na kupewa mkataba na Wizara wa kusambaza chanjo kwa wafugaji ambapo kwa sasa amekabidhi majokofu 60 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya zoezi hilo.
Bw. Gandhi alitaja malengo ya Kampeni ya uchanjaji Kitaifa ni kuondoa vikwazo vya biashara ya Mifugo na mazao yake Kikanda, Kimataifa kwa kutokomeza ugonjwa wa mapafu ya Ng'ombe (CBPP), Ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na kondoo (PPR) na kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Kideri, Ndui na Mafua ya Kuku.