Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MAFUNZO YA WATAALAMU WA AFYA YA MIFUGO KIMATAIFA, YAZINDULIWA

Imewekwa: 19 May, 2025
MAFUNZO YA WATAALAMU WA AFYA YA MIFUGO KIMATAIFA, YAZINDULIWA
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imezindua rasmi mradi wa mafunzo kwa wataalamu wa afya ya mifugo, yanayofanyika katika nchi nne za Tanzania, Botswana, Zambia na Malawi. Akizungumza leo (Mei 17, 2025) wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mafunzo maalum kwa wataalam hao uliofanyika katika Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema mafunzo hayo yamelenga kuwapa ujuzi wa kisasa vijana, hususan wahadhiri ili waendane na hali halisi ya sekta ya ufugaji ndani na nje ya nchi. Akizungumzia juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Prof. Shemdoe amesema Serikali iinaanzisha Kampeni ya Chanjo Kitaifa kwa ajili ya magonjwa 13 sugu ya mifugo itakayozinduliwa mwaka huu. “Kampeni hiyo itaanza na magonjwa matatu, ambapo ng’ombe milioni 19, mbuzi na kondoo milioni 17, pamoja na kuku milioni 40 wanatarajiwa kuchanjwa nchi nzima. ” amesema Prof. Shemdoe. Aidha, amebainisha kuwa kampeni hiyo itaambatana na mpango wa utambuzi wa mifugo kwa kuweka hereni kwa mifugo ili kutambua waliopata chanjo na mahali walipo. “Hii itamsaidia mfugaji kwenye ufuatiliaji wa afya ya mifugo wake na pia kufungua fursa katika masoko ya kimataifa,” ameongeza Prof. Shemdoe. Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene, amesema baadhi ya wahadhiri watapatiwa mafunzo ndani ya nchi, huku wengine wakipewa fursa ya kwenda Hungary, Slovakia na Ubelgiji kwa ajili ya mafunzo ya juu na utaalamu katika maeneo yanayohusiana na afya ya mifugo. Washiriki wa mafunzo haya ni pamoja na wataalamu kutoka halmashauri za wilaya, manispaa na majiji, pamoja na wahadhiri na wanafunz i wa LITA. Mafunzo haya yameandaliwa kupitia mradi wa EDVET unaosimamiwa na Shirika la MIOUT, kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nchi za Hungary, Finland na Slovakia.
Mrejesho, Malalamiko au Wazo