​KUFUNGWA KWA SHUGHULI ZA UVUVI NI LAZIMA KUSHIRIKISHE WANANCHI-SERIKALI

Imewekwa: Tuesday 28, September 2021

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) imesema kuwa mfumo unaohusisha kupiga marufuku uendeshaji wa shughuli za uvuvi katika baadhi ya maeneo ya maziwa, mito na bahari ni lazima uhusishe wananchi kwa sababu ndio wanufaika na waaathirika wa marufuku hiyo.

Hayo yamesemwa leo (16.09.2021) na Mkurugenzi wa Uvuvi nchini Bw. Emanuel Bulayi alipokutana na timu ya watendaji kutoka Shirika la kimataifa la “The nature conservancy” katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo uliopo eneo la Mtumba jijini Dodoma.

Bulayi ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu (Uvuvi) amesema kuwa hatua hiyo hutokana na viashiria vya hali ya kutoweka kwa aina flani ya samaki au kupungua kwa idadi ya samaki katika vyanzo hivyo.

“Jambo hili lipo kisheria kabisa na hata nyie “Tuungane” kabla hamjatekeleza hilo ni lazima mhakikishe wananchi pamoja na wawakilishi wao wameshirikishwa ipasavyo na wameridhia na bahati nzuri mkiwajengea uelewa mzuri wanatoa ushirikiano mfano tunaona kule Songosongo ambapo huwa tunafunga uvuvi wa pweza na kwa kweli tumeona faida yake” Amesema Bulayi.

Akizungumzia kuhusu ombi la shirika hilo kufanya sensa ya uvuvi katika sehemu ya Ziwa Tanganyika, Bulayi amesema kuwa Wizara yake hairuhusu jambo hilo kwa sababu litasababisha kupatikana kwa taarifa zisizo sahihi katika baadhi ya maeneo na hivyo kuipotosha Serikali katika utekelezaji wa shughuli zake kwa upande wa Ziwa Tanganyika.

“Nakubaliana na nyie kuwa takwimu za mwaka 2011 tulizonazo hazifai tena kutumika kufanya tathmini ya shughuli za Uvuvi wa Ziwa Tanganyika na ndio maana lengo letu ni kukusanya takwimu za Ziwa lote na si sehemu pekee hivyo nashauri mtujulishe kiasi mlichonacho ili nasi tuangalie namna gani tunaweza kufanikisha kufanya zoezi hilo kwa Ziwa lote badala ya sehemu tu kama mlivyokuwa mnataka” Ameongeza Bulayi.

Kwa upande wake Lukindo Hiza ambaye ni Mkurugenzi wa mradi wa “Tuungane” unaotekelezwa na Shirika hilo kwa lengo la kuboresha uvuvi wa Ziwa Tanganyika ameishukuru Wizara kwa ushiriki wake wakati wote wa utekelezaji wa mradi huo ambapo ameahidi kufanyia kazi maelekezo yote waliyopewa na Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu.

“Kwenye hili la kufunga shughuli za uvuvi kwa lengo la kuongeza wingi wa samaki tutaenda kuwashirikisha wavuvi na wawakilishi wao kama ulivyotuagiza na baada ya hapo tutaleta mrejesho kama wameridhia au la” Amesema Hiza.

Naye Mkurugenzi wa Uvuvi wa Ziwa Tanganyika kutoka Shirika hilo, Limbu Peree ameiomba Wizara kuwapa mpango mkakati wake kuhusiana na uvuvi wa Ziwa Tanganyika ili waweze kuunganisha na ule walionao kwa lengo la kuhakikisha mikakati yao na ya Wizara haikinzani.

“Kama tukiwa na hii “workplan” ya Wizara na Wizara wakawa na ya kwetu itatusaidia kuzungumza lugha moja na kutopishana masuala mbalimbali ya kiutekelezaji kwa upande wa Ziwa Tanganyika” Amesema Limbu

Mradi wa “Tuungane” ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa kwa upande wa Ziwa Tanganyika kwa lengo la kuboresha shughuli za uvuvi zinazotekelezwa katika ziwa hilo.

.