KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA USIMAMIZI FEDHA ZA UJENZI WA GHALA LA MALISHO MPWAPWA.

Imewekwa: Friday 21, March 2025

KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA USIMAMIZI FEDHA ZA UJENZI WA GHALA LA MALISHO MPWAPWA.

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara,Kilimo na Mifugo imeipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa usimamizi mzuri wa fedha takribani Shilingi Milioni 219.7 zilizotumika kwenye ujenzi wa Ghala la kuhifadhia malisho ya Mifugo Wilayani Mpwapwa, Dodoma.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Deodatus Mwanyika mara baada ya kuiongoza kamati yake kukagua Ghala hilo ambalo kukamilika kwake kutaifanya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kuhifadhi zaidi ya marobota 30,000 kwa wakati mmoja tofauti na awali ambapo maghala yake yaliweza kuhifadhi marobota 14,000 pekee.

“ Sisi tunawapongeza sana Wizara kupitia Taasisi ya TALIRI kwa kazi mliyofanya hapa, “its a sound structure” mmefanya vizuri lakini tukupongeze Mhe. Waziri kwa sababu mkandarasi wa hapa pia amefanya kazi nzuri hivyo tunaweza kusema usimamizi wa Wizara hii kwenye miradi upo vizuri” Amesema Mhe. Mwanyika.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji mbali na kuishukuru kamati hiyo kwa kuidhinisha bajeti iliyowezesha ujenzi wa ghala hilo, ameliahidi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kusimamia fedha zote zinazoidhinishwa Wizarani hapo ili kuongeza tija kwa wafugaji na wavuvi.

Aidha Dkt. Kijaji amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha kwa vitendo dhamira yake ya kufanya mapinduzi kwenye sekta za uzalishaji ikiwemo Mifugo ikiwa ni pamoja na kuwezesha kupatikana kwa mbegu bora za mifugo na malisho ya mifugo hiyo.

Akielezea lengo la ujenzi wa ghala hilo Mkurugenzi wa Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Dkt. Asimwe Rwiguza amesema kuwa mradi huo utasaidia upatikanaji wa malisho kwenye kituo hicho kwa kipindi chote cha mwaka, kulinda ubora na kupunguza upotevu wa malisho hayo kutokana na kukosekana sehemu sahihi ya kuyahifadhi.

.