KAMANI ATAJA MIKAKATI YA SERIKALI KUONGEZA MAENEO YA MALISHO
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza kutekeleza mkakati wa miaka mitano wa kuongeza maeneo kwa ajili ya shughuli za ufugaji kwa kutenga hekta milioni 2.51, ikiwa ni sehemu ya kuongeza maeneo yaliyopimwa na kutengwa kwa shughuli za ufugaji kutoka hekta milioni 3.49 hadi hekta milioni sita kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025- 2030 na hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa kufungua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwezi Novemba 14, 2025.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani leo Januari 28, 2026 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu Swali la Mbunge wa Ngorongoro Mhe. Yannick Ikae Ndoyinyo lililohoji serikali inampango gani wa kuongeza maeneo ya malisho kutoka hekta milioni Tatu hadi hekta milioni sita kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inavyosema?.
“Mhe. Spika Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wizara, idara na taasisi zenye majukumu ya kisheria ya kupanga na kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi tumeanza kuandaa mkakati wa miaka mitano wa kutenga hekta milioni 2.51 kwa ajili ya shughuli za ufugaji, wakati wa utekelezaji wa mkakati huu waheshimiwa wabunge wote watashirikishwa” alisema Mhe. Kamani.
Aidha, Mhe. Kamani amesema wizara itaendelea kutoa taarifa na elimu kwa wafugaji kote nchini kupitia vyombo vya habari kuhusu mabadiliko ya tabianchi ili kuwasaidia wafugaji kuchukua tahadhari ya kuikinga mifugo yao, pia katika kutafuta unafuu wa changamoto ya malisho serikali imeshusha bei ya mbegu za malisho kutoka shilingi 4,000 kwa kilo hadi shilingi 1,000.