Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

KAMANI AINADI MAMLAKA YA UVUVI BUNGENI

Imewekwa: 28 January, 2026
KAMANI AINADI MAMLAKA YA UVUVI BUNGENI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani amelieleza Bunge kuwa katika kukabiliana na changamoto ya Uvuvi usiofuata sheria Serikali kupitia Wizara yake ipo kwenye hatua za mwisho za kuanzisha mamlaka ya Uvuvi itakayofanikisha kudhibiti changamoto hiyo kwenye maeneo yote ya Uvuvi nchini.

Mhe. Kamani amesema Januari 27,2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya wabunge mbalimbali waliotaka kufahamu hatua ambazo Serikali imechukua katika kudhibiti vitendo vya Uvuvi usiofuta Sheria ambapo amesema kuwa hatua hiyo itarahisisha utekelezaji wa Mpango kabambe wa sekta ya Uvuvi wa mwaka 2021-2037 wenye kipumbele cha kuanzisha, kufufua, kuendeleza na kuimarisha viwanda vya kuchakata mazao ya Uvuvi nchini.

“Mhe. Spika ili kuhakikisha viwanda vyetu vinafanya kazi kulingana na matarajio ya Serikali, Wizara ipo katika hatua za maamuzi kulingana na taratibu za Serikali  kuanzisha mamlaka ya Uvuvi kwa lengo la Usimamizi wa rasilimali za Uvuvi na kupambana na Uvuvi usiozingatia sheria” Amesema Mhe. Kamani.

Aidha Mhe. Kamani amebainisha hatua za awali ambazo Wizara yake imezitekeleza ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa malighafi ya samaki ikiwa ni pamoja na kuweka maboya 32 yenye thamani ya shilingi milioni 224 katika eneo la Uchelele mkoani Mwanza.

Mhe. Kamani ameongeza kuwa Wizara yake imeendelea kuhamasisha ufugaji samaki kwa njia ya Vizimba ili kuongeza kiwango cha upatikanaji wa samaki na kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi kwenye viwanda.

Akijibu swali linalohusiana na mikakati ya Serikali kwenye ujenzi wa Viwanda vya nyama, Mhe. Kamani amesema kuwa Wizara yake inaendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili wawekeze kwenye eneo hilo huku pia akisisitiza kuendelea kuhamasisha wafugaji wote nchini kufuga kisasa ili viwanda hivyo viweze kupata mazao yenye ubora

Mrejesho, Malalamiko au Wazo