JENGO LA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI NI LA MFANO-KAMATI YA BUNGE

Imewekwa: Friday 21, March 2025

JENGO LA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI NI LA MFANO-KAMATI YA BUNGE

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imepongeza hatua ya ujenzi wa Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi unaoendelea kwenye eneo la Mtumba jijini Dodoma ambapo imetaja jengo hilo kuwa la mfano ukilinganisha na mengine.

Pongezi hizo zimetolewa Machi 20, 2025 na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Mariam Ditopile muda mfupi baada ya kuiongoza kamati yake kukagua jengo hilo litakalogharimu takribani Bil. 24.9 hadi kukamilika kwake.

"Kwa niaba ya kamati nzima kwa kweli niipongeze sana Wizara kwa sababu tumejionea jengo hili limekidhi vigezo vyote vya kitaalam lakini wamejiongeza limekuwa la kisasa mno na tumeoneshwa miundombinu ya gesi na maji kwa ajili ya kuzima moto na wamekidhi pia vigezo kwa kuweka miundombinu kwa watu wenye mahitaji maalum" Amesema Mhe. Ditopile.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji mbali na kuishukuru kamati kwa ushirikiano waliowapa wakati wote wa ziara amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizotumika kujengea ofisi hiyo ambapo ameahidi Wizara yake kuendelea kutoa huduma bora zaidi mara watakapohamishia shughuli zao kwenye jengo hilo.

"Sisi kama Wizara tumejisikia faraja sana kwa sababu wabunge ni wawakilishi wa wananchi hivyo tunaona jicho la wananchi limeridhika na kazi yetu" Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji.

Naye mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo Mhe. Eng. Ezra Chiwelewa ametoa rai kwa Taasisi nyingine kuwa na imani kwa wakandarasi wazawa kama walivyofanya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambao wametekeleza mradi huo kwa viwango bora.

Akizungumzia hatua za ujenzi zilizosalia kwenye jengo hilo, Mbunifu majengo kutoka Wakala ya Majengo nchini (TBA) ambaye ndio mshauri mwelekezi wa mradi huo Bw. Jona Mgogo amesema kuwa mpaka sasa wamefikia asilimia 93 ya ujenzi wa Jengo hilo ambapo amebainisha kuwa kazi kubwa iliyosalia ni umaliziaji wa utengenezaji wa Tanki la kubwa la kuhifadhia maji chini ya jengo na uwekaji wa vioo.

.