Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

FETA YAZINDUA MAFUNZO YA KOZI FUPI KADA YA UJUZI WA UVUVI

Imewekwa: 21 May, 2025
FETA YAZINDUA MAFUNZO YA KOZI FUPI KADA YA UJUZI WA UVUVI
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kupitia Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), imezindua Mafunzo ya Kozi fupi za Uvuvi na kuboresha Miundombinu ya Kampasi hiyo ya Gabimori, ikiwa ni pamoja na kujenga Madarasa mawili kwa ajili ya Mafunzo, Miundombinu ya msingi ya vitotoleshi vya Vifaranga vya Samaki, Vizimba viwili vya kufugia Samaki, Recirculating Aquaculture System (RAS), na Birika la kunyweshea Mifugo. Akizungumza wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Miundombinu na Upandikizaji wa vifaranga vya samaki kwa ajili ya kuanza kutoa mafunzo katika Kampasi ya FETA Gabimori, leo Mei 20, 2025 Rorya - Mara, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede amesema kuwa FETA inaanzisha Rasmi Mafunzo ya Kozi fupi katika Kampasi ya Gabimori ili wananchi waweze kujifunza jinsi ya kufuga Samaki kwa njia ya Vizimba na mabwawa. “Leo tunazindua Programu za Mafunzo ya Kozi fupi hapa FETA Gabimori ili ianze kuwanufaisha wanajamii wanaozunguka eneo hili na wengine kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo nje na Mkoa wa Mara ili waweze kujifunza shughuli za Uvuvi na ukuzaji viumbe maji. ameseama Dkt. Mhede Dkt. Mhede amesema kuwa Vifaranga vilivyopandikiza ni 35,000, ambapo vifaranga 4,000 vimepandikizwa kwenye vizimba viwili vya mafunzo ya vitendo, na kwenye bwawa (lambo) vimepandikizwa vifaranga 31,000 vyenye gramu kumi mpaka kumi na tano katika bwawa lenye ujazo wa waji lita milioni kumi. Vilevile, Dkt. Mhede amesema kuwa vifaranga vya samaki vitakuwa vinazalishwa FETA Kampasi ya Gabimori ili wale watakaokuwa wameanzisha vikundi vya miradi ya Ufugaji samaki kwa njia ya vizimba waweze kupata vifaranga kwa gharama himilivu. Dkt. Mhede amesema kinachofanyika ni muendelezo wa Muongozo wa Serikali katika namna ya kutumia rasilimali za maji ili kuongeza kipato zaidi kwa jamii na uchumi wa nchi nzima ambapo Serikali ina mpango wa kupandikiza Vifaranga vya Samaki kwenye vyanzo mbalimbali vya maji nchi nzima. Aidha, Dkt. Mhede amebainisha kuwa, FETA Gabimori kuna mradi unganishi ambao unahudumia pia Mifugo ambapo kuna Birika la kunyweshea Mifugo na Miundombinu ya Uvuvi. Naye, Mtendaji Mkuu wa FETA, Dkt. Semvua Mzighani, amesema kuwa miundombinu ambayo imejengwa itasaidia Kampasi ya Gabimori kutoa Mafunzo ya Muda mfupi na ya muda mrefu (pale ambapo miundombinu yote ya chuo itakuwa imekamilika). Dkt. Mzighani amesema kuwa FETA Gabimori itajikita katika kuwafundisha wananchi uzalishaji wa samaki kuanzia kwenye vifaranga mpaka pale samaki anapofika sokoni au kwenda kuliwa. Halikadhalika, Dkt. Mzighani amebainisha kuwa wananchi watajifunza mbinu zote za uzalishaji wa vifaranga vya samaki pamoja na chakula bora cha samaki, na jinsi ya kuwatunza samaki pamoja na kupima ubora wa samaki ikiwemo jinsi ya kupata masoko na kuchakata samaki. Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Mara, ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji, Mhandisi Mwita Chacha Okayo, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuwataka wananchi wajitokeze kwa wingi ili waweze kupata mafunzo ya Ufugaji Samaki katika Chuo cha FETA Kampasi ya Gabimori.
Mrejesho, Malalamiko au Wazo