Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

DKT. KIJAJI AKABIDHI BOTI ZA UVUVI ZENYE THAMANI YA BIL.2

Imewekwa: 21 July, 2025
DKT. KIJAJI AKABIDHI BOTI ZA UVUVI ZENYE THAMANI YA BIL.2

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amekabidhi boti 13 za Uvuvi zenye thamani ya takribani shilingi Bil. 2 kwa Vikundi vya mikoa ya Pwani na Dar-es-salaam ambazo zinatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya Wavuvi 205  wa mikoa hiyo.

Mhe. Dkt. Kijaji amekabidhi boti hizo Julai 16, 2025 kwenye ufukwe wa Shirika la Uvuvi nchini (TAFICO) ambapo mkoa wa Pwani umekabidhiwa Boti 8 huku mkoa wa Dar-es-Salaam ukikabidhiwa boti 5 zote jumla zikiwa na uretu wa mita 12 na 14 ambazo zinajumuisha vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Nyavu, kamba, maboya, nyuzi, kitafuta samaki na boti saidizi maarufu kama dingi.

“Boti mlizopokea leo zimefanyiwa maboresho yote yaliyotokana na maoni mliyotoa kutoka kwenye boti za awamu ya kwanza na sisi kama Serikali tunatamani kuona mnaendelea mnafanikiwa kupitia boti hizo” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji

Aidha Mhe. Dkt. Kijaji amebainisha kuwa ugawaji wa boti hizo ni sehemu ya mkakati wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan uliolenga kuboresha sekta ya Uvuvi nchini ambapo wanufaika wanajumuisha makundi manne ambavyo ni watu binafsi, makampuni na vikundi vya Wavuvi.

“ Boti hizi zimechangia ongezeko la idadi ya watu wanaonufaika kutokana na Sekta ya Uvuvi ambapo mpaka zaidi zaidi ya Watu Milioni 6 wanapata vipato vyao kupitia sekta hii hivyo niwaombe wote mliopatiwa mikopo hii muirejeshe kwa wakati ili tuwawezeshe na wengine kukopeshwa “ Amesema Mhe. Dkt. Kijaji.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Mikaya Dalmia amesema kuwa awamu ya kwanza ya mkopo wa boti hizo za Uvuvi iliufanya mkoa huo kuvuna takribani tani 18892 za samaki hivyo aliwataka wanufaika wa awamu ya pili kutumia vema fursa hiyo ili wavune zaidi ya kiwango hicho cha awamu iliyopita.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Shaib Ndemanga mbali na kuishukuru Serikali kwa boti hizo zinazotolewa kwa mkopo wenye masharti nafuu, amesema kuwa zitaboresha maisha ya wananchi wa mkoa huo ambao kwa kiasi kikubwa wanajishughulisha na shughuli za Uvuvi kwa ajili ya mahitaji ya Chakula na kukuza uchumi wao.

Boti hizo zilizotolewa leo ni sehemu ya Boti 120 zinazotarajiwa kutolewa kwenye awamu ya pili ya Mkopo huo wenye masharti nafuu ambapo mpaka kukamilika kwa awamu zote mbili jumla ya Boti 280 zinatarajiwa kukopeshwa kwa Wavuvi nchini.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo