DKT. BASHIRU ATAKA KASI UTAFITI WA MIFUGO, AIPA MAAGIZO TALIRI
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kuongeza kasi ya kufanya tafiti katika maeneo ya afya, malisho na mbari za mifugo ili taasisi hiyo iwe kitovu cha uhimilishaji na uhaulishaji kwa kanda ya kati.
Mhe.Balozi Dkt. Bashiru ametoa agizo hilo leo Oktoba 27, 2026 Wilayani Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma wakati wa ziara yake TALIRI Kanda ya Kati, iliyolenga kukagua shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo pamoja na kubaini changamoto zake.
Pamoja utafiti huo ameiagiza TALIRI kuandaa mpango wa makisio ya bajeti kwa kuzingatia mahitaji ya maabara itakayotumika kwa ajili ya uhimilishaji na uhaulishaji wa mifugo ili mabadiliko ya uboreshaji wa mbegu na sekta ya mifugo yaonekane na kuifanya TALIRI kuwa kitovu cha utafiti na uzalishaji wa mifugo.
Katika hatua nyingine Waziri Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amepiga marufuku utaratibu wa uuzaji wa mbegu za malisho kwa ajili ya biashara na badala yake mbegu hizo zenye ruzuku ya serikali ziwanufaishe wafugaji ambapo amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara Hiyo, kuandika waraka utakaotoa mwongozo mpya wa kuuza mbegu hizo.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Dkt. Sophia Mfaume Kizigo amesema kampeni ya elimu ya uhamasishaji wa kilimo cha malisho inahitajika kufikishwa kwa wafugaji ngazi ya chini ili kuwajengewa uelewa wa kilimo hicho, hatua itakayosaidia kupunguza migogoro ardhi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Anayeshughulikia sekta ya mifugo, Dkt. Fabian Madele, kwa niaba ya Katibu Mkuu ameahidi kufanyia kazi maelekezo aliyoyatoa waziri kwa ushirikiano na wataalam kutekeleza kwa vitendo mageuzi ya sekta hiyo pamoja na kutekeleza Dira ya Maendeleo 2050.
Awali, Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania Dkt. Kabudi Kabudi alimweleza Waziri kuwa TALIRI inahitaji kuwezeshwa kuwa na Maabara ya Kisasa kwa ajili ya Uhimilishaji na Uhaulishaji wa Mifugo kwa kushirikiana na Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) ili matokeo ya tafiti za mifugo yatumike kwa vitendo katika kuongeza uzalishaji.