Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

DKT. BASHIRU AFANYA MAZUNGUMZO NA FAO KUENDELEZA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI

Imewekwa: 30 January, 2026
DKT. BASHIRU AFANYA MAZUNGUMZO NA FAO KUENDELEZA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amekutana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika  la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Nchini Tanzania Dkt. Nyabenyi Tipo  na kufanya mazungumzo yanayolenga kuendeleza ushirikiano  katika kukuza na kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi nchini.

Kikao hicho kimefanyika leo Januari 29, 2026 katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi  zilizopo Kambarage Tower Jijini Dodoma ambapo Mwakilishi Mkazi wa FAO nchini Tanzania Dkt. Tipo ametumia nafasi hiyo, pia kujitambulisha na kumpongeza Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kukurwa kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Akizungumza Katika kikao hicho Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amesema serikali ya awamu ya sita imetoa kipaumbele kwenye bajeti kwa sekta za uzalishaji ikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi, hivyo juhudi zinazofanywa na FAO katika  sekta za  uzalishaji ni  ishara ya kuimarisha uchumi wa wananchi, na kumhakikishia Dkt. Tipo kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi  na FAO zitaendelea kushirikiana  katika kuendeleza sekta hiyo ili kuimarisha uchumi wa wananchi na usalama wa chakula .

Naye, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO)  Dkt. Nyabenyi Tipo amesema Tanzania imendelea kupiga hatua katika kuchangia  ukuaji wa pato la taifa kupitia sekta za uzalishaji na kamba FAO itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa kutoka asilimia 5 ya sasa hadi kufikia asilimia 6.5 katika mwaka unakuja.

FAO imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika sekta za mifugo na uvuvi ikiwemo udhibiti wa magonjwa kupitia mpango wa utoaji chanjo, miradi ya ukuzaji viumbe maji pamoja na uwezeshaji wa wafugaji na wavuvi kuongeza uzalishaji na usalama wa chakula.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo