Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

DKT. BASHIRU AAGIZA KUUNDWA KWA CHOMBO CHA KUUNGANISHA WASAFIRISHAJI WA NYAMA NJE YA NCHI

Imewekwa: 12 January, 2026
DKT. BASHIRU AAGIZA KUUNDWA KWA CHOMBO CHA KUUNGANISHA WASAFIRISHAJI WA NYAMA NJE YA NCHI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally amemwagiza Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania kukutana na wawekezaji wanaosafirisha nyama nje ya nchi ili kuunda chombo kitakachowaunganisha  kwa ajili ya uendeshaji wa biashara ya nyama kimataifa na kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji hao.

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally ametoa agizo hilo  Januari 8, 2026 baada ya kutembelea Kiwanda cha Nyama cha Chobo Investment Company kilichopo Usagara mkoani Mwanza, ambapo amesema ili changamoto za wawekezaji ziweze kutatuliwa  ni muhimu kuwa na umoja kwa wawekezaji hao.

" Serikali haiwezi kutatua changamoto za mwekezaji mmoja mmoja, sasa Msajili wa Bodi ya Nyama, kwahiyo maelekezo yangu pamoja na chombo hicho, nitayarishie kikao na wauzaji wa nyama nje ya nchi kati kati ya mwezi wa pili, kile kikao ndio kitazaa umoja wa chombo imara " alisema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha,  Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amemwangiza Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania kwa kushirikia na Idara ya Uzalishaji na Masoko (DPMD) kuunda timu ya wataalam itakayofanya mapitio ya mradi na shughuli zinazotelezwa na Kiwanda cha Chobo Investment  Company ili  kutathmini sababu zilizomsababishia  mwekezaji kuchelewe kuanza uzalishaji.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho  Bw. John Chobo amesema wawekezaji wanakumbana na changamoto mbalimbali wanaposafirisha nyama nje ya nchi hivyo amependekeza usafirishaji wa nyama uwe unafanyika ukiwa kwenye taswira ya nchi.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo