DC NZEGA AWAKARIBISHA WATANZANIA KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA KICHAA CHA MBWA
Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mhe. Naitapwaki Tukai, amewaalika wananchi wa Nzega na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani kitakachofanyika kesho Septemba 28, 2026 katika viwanja vya Mwanhala, Wilayani Nzega Mkoani Tabora.
Kutokana na juhudi mbalimbali ikiwemo utoaji wa chanjo ya kichaa cha mbwa, kumekuwa na mafanikio makubwa ya kupunguza matukio ya ugonjwa huo Wilayani humo, kutoka matukio 315 mwaka 2021 hadi kufikia matukio 75 tu mwaka 2026, ameyasema hayo Leo Septemba 27, 2026 Nzega.
"Niwaombe wananchi kutunza mbwa kwa kuwapa chanjo ili kuweza kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza kwa binadamu. Kesho siku ya maadhimisho chanjo itatolewa sambamba na kufunga vizazi ili kuzuia mbwa kuzaa kiholela, na elimu itatolewa kwa kina," amesema Mhe. Tukai.
Aidha, Mhe. Tukai amesisitiza umuhimu wa kuwafundisha watoto namna ya kumtunza mbwa ili kupunguza idadi ya mbwa wanaozurura mitaani na kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza.
Maadhimisho hayo kitaifa yanafanyika Wilayani Nzega na yanabebwa na kaulimbiu isemayo "Kwa pamoja tuna nguvu zaidi".