Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

CHANJO YA MIFUGO ITAONGEZA THAMANI YA MIFUGO YETU - DKT. MHEDE

Imewekwa: 21 July, 2025
CHANJO YA MIFUGO ITAONGEZA THAMANI YA MIFUGO YETU - DKT. MHEDE

Uamuzi wa Serikali wa kuwekeza kwenye sekta ya mifugo kwa kutoa ruzuku ya chanjo na utambuzi wa mifugo utasaidia kupatikana kwa  ithibati kutoka Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH) ya kufanya biashara ya mifugo na mazao yake kwenye masoko ya ndani na ya kimataifa jambo litakaloinua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Hayo yamefahamika wakati Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede akikagua utekelezaji wa Kampeni ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo  katika kijiji cha Soera wilayani  Kondoa mkoani Dodoma leo Julai 21, 2025.  

"  Leo tumekabidhi pikipiki 31 kwa maafisa ugani ili waweze kutekeleza kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo, serikali imetoa ruzuku ya chanjo ya asilimia 50 kwa ng'ombe, mbuzi na kondoo na asilimi 100 (bure) kwa chanjo ya kuku kwahiyo chanjo  hii itaongeza thamani ya mifugo yetu" amesema Dkt. Mhede.

Kuhusu utambuzi Dkt. Mhede amesema zoezi la chanjo ya mifugo linaenda sambamba na utambuzi ili  kutengenisha  mifugo iliyochanjwa na ambayo bado haijachanjwa na kudhibiti wizi wa mifugo na kutoa wito kwa wataalam wanaoenda kutekeleza kampeni hiyo kutumia na kuvitunza vifaa vya chanjo  ili viwahudumie wafugaji kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Bi. Mwasiti  Juma ameishukuru serikali kwa kutoa chanjo hiyo kwani itawainua wafugaji kiuchumi kutokana na kwamba sekta ya mifugo ni sehemu muhimu katika uchumi wa Kondoa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Shabani Millao amekiri kuipokea kampeni hiyo na kuahidi kuwasimamia wataalam wa chanjo na utambuzi wa Mifugo kutekeleza kampeni hiyo kwa wafugaji wote wa Wilaya hiyo.

Naye Daktari wa Mifugo Wilaya Kondoa ambaye ndiye mratibu wa kampeni ya chanjo na utambuzi Wilayani hapo Dkt. Chritian Mwiga amesema wilaya hiyo itachanja ng'ombe 200,000 mbuzi na kondoo 280,000 na kuku 460,000 huku akitoa wito kwa wafugaji kupeleka mifugo katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya chanjo.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo