CHANJO NA UTAMBUZI KUIWEZESHA MIFUGO KUPATA BIMA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo inayoendelea nchini itawawezesha wafugaji kupata bima ya Mifugo yao.
Mhe. Dkt. Kijaji amesema hayo Julai 06, 2025 wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa utekelezaji wa kampeni hiyo Wilaya ya Chato mkoani Geita ambapo ametoa rai kwa wafugaji hao kuchanja na kutambua mifugo yao yote ili waweze kunufaika na huduma hiyo.
“Huko nyuma wafugaji walikuwa wakilalamika mifugo yao kufa kwa kukosa malisho, Mhe. Rais ameiwezesha mifugo yote kukatiwa bima kwa kuwa itakuwa imeshafanyiwa utambuzi” Amesema Mhe. Dkt. Kijaji
Mhe. Dkt. Kijaji ameongeza kuwa zoezi hilo ni la miezi 2 hivyo amewasihi wafugaji kuhakikisha mifugo yao yote imechanjwa na kutambuliwa ndani ya kipindi hicho ” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji
Akigusia faida za utambuzi wa Mifugo Mhe. Dkt. Kijaji amesema kuwa zoezi hilo litawasaidia wafugaji kuondokana na changamoto wa wizi wa Mifugo yao kwa kuwa kila mfugo utatambuliwa kwa nambari maalum zinazopatikana kwenye hereni za kielektroniki.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela ameipongeza Wizara na Serikali kwa ujumla kwa kuwawezesha wataalam wa Mifugo mkoani kwake vitendea kazi vinavyowawezesha kuwahudumia wafugaji kwa urahisi.
“Chanjo hii ni salama kwa asilimia 100 na ndio maana miongoni mwa Mifugo iliyopata chanjo leo ni pamoja na ile ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na ya Naibu Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Doto Biteko na nikuhakikishie Mhe. Waziri sisi Geita tutahakikisha tunafikisha zaidi ya asilimia 70 ya Mifugo yote ndani ya miezi hii miwili ya kampeni” Amesema Mhe. Shigela
Ziara hiyo ya Mhe. Dkt. Kijaji iliyolenga kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo iliyozinduliwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Juni 16, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Tabora na Dodoma.