CHANJA ZENYE THAMANI YA MILIONI 117 ZATOLEWA KWA WAVUVI KILWA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) imewawezesha wavuvi wa dagaa waliopo eneo la Kilwa Kivinje mkoani Lindi Chanja 40 za kisasa za kuanikia dagaa zenye thamani ya shilingi Mil. 117.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi chanja hizo iliyofanyika Agosti 21,2025 Wilayani Kilwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa tukio hilo ni sehemu ya mkakati wa Serikali unaolenga kuondokana na changamoto ya upotevu wa mazao ya Uvuvi baada ya kuvunwa na kuhakikisha dagaa zinazovuliwa kwenye eneo hilo zinakaushwa kwenye mazingira yanayozingatia usalama wa chakula.
“Natambua kuwa hapo awali dagaa mnaovua hapa walikuwa wakiharibika kutokana na kukaushiwa kwenye miundombinu isiyo rafiki na wakati mwingine walikuwa wakikutwa na mchanga au matope jambo ambalo mbali na kupunguza thamani ya mazao hayo sokoni lilikuwa likihatarisha afya za walaji hivyo hatua hii itamaliza changamoto hizo zote” Amesema Mhe. Dkt. Kijaji.
Aidha Mhe. Dkt. Kijaji amewataka wanufaika wa miundombinu hiyo kuhakikisha wanaitunza na kuitumia kama ilivyokusudiwa ili iweze kuwanufaisha kwa muda mrefu zaidi na kukidhi malengo ya kutolewa kwake.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack ameishukuru Serikali na Shirika la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwa kuwawezesha wavuvi wa mkoa wake miundombinu hiyo ambapo mbali na kuahidi kusimamia matumizi yake amewataka wavuvi hao kuhakikisha wanakuza uchumi wao kupitia chanja hizo.
“Ndoo moja ya dagaa wabichi sasa inauzwa kati ya shilingi elfu 40 hadi elfu 45 na dagaa wavuvi wetu wanauza kwenye nchi za Rwanda, Congo na Burundi hivyo hatukuwa na tatizo la soko bali ilikuwa namna ya kuongeza thamani ya mazao yetu jambo ambalo leo limeanza kushughulikiwa kupitia ugawaji wa chanja hizi” Ameongeza Mhe. Telack.
Mbali na Chanja hizo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha mazingira ya shughuli za Uvuvi nchini ikiwa ni pamoja na kujenga masoko na maghala ya kuhifadhia samaki, vyumba vya kuhifadhi ubaridi, mitambo ya kuzalisha samaki na teknolojia za ukaushaji wa mazao ya uvuvi.