BI. MEENA AFUNGUA WARSHA YA UJUMUISHAJI BIOANUWAI KATIKA USIMAMIZI WA UVUVI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena amefungua warsha ya ujumuishaji wa masuala ya bioanuwai katika usimamizi wa uvuvi nchini iliyowakutanisha takribani washiriki 50 katika Hoteli ya Giraffe Jijini Dar es Salaam wakiwemo watafiti, wawakilishi wa halmashauri za wilaya, wataalam wa uvuvi wa ndani na wa kimataifa, asasi za kiraia, wawakilishi wa wavuvi wadogo na wadau wa maendeleo.
Akifungua warsha hiyo leo Oktoba 7, 2025, Bi. Meena amewahimiza washiriki hao kuzitambua changamoto zinazoikabili mifumo ya Bioanuwai ili kulinda rasilimali za uvuvi nchini.
"Ndugu washiriki tunapojadili ujumuishaji wa bioanuwai katika usimamizi wa uvuvi, ni muhimu kutambua changamoto zinazoikabili mifumo ya ikolojia nchini ukiwemo uvuvi haramu ambao umesababisha kupungua kwa samaki na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa yakibadilisha makazi ya viumbe na kuvuruga mifumo ya uzalishaji wa samaki mambo haya yanatishia bioanuwai na ustawi wa jamii." Alisema Bi. Meena.
Alisema ili kukabiliana na changamoto hizo kunahitajika ushirikiano wa pamoja utakaoleta mikakati ya namna bora ya ujumuishaji katika uhifadhi wa bioanuai katika mifumo ya usimamizi ya uvuvi kwa kuzingatia misingi ya uendelevu wa rasilimali ya Uvuvi.
Kwa upande Wake Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) nchini Tanzania Dkt. Nyabenyi Tipo amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Tanzania katika kujumuisha Bioanuwai kwenye usimamizi wa sekta ya uvuvi kwa kugusa kundi la vijana na wanawake kunufaika na sekta hiyo kwa kuwa na usalama wa chakula na ajira.
"Ajenda hii inaakisi jukumu kuu la FAO la kuendeleza uvuvi endelevu na mchango wetu wa pamoja katika juhudi za kimataifa za kupunguza umaskini na kujenga mifumo imara ya chakula. Pia inaendana kikamilifu na Mwongozo wa Hiari wa Kuhakikisha Uvuvi Endelevu wa Wavuvi Wadogo, ambao unatoa wito wa usimamizi wa kuwajibika wa rasilimali za uvuvi na kuwawezesha wavuvi wadogo, wanawake na vijana ambao wako katika kiini cha sekta hii" alisema Dkt. Tipo.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uvuvi nchini ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi Bw. Christian Nzowa amesema asilimia 40 ya mazao ya uvuvi hupotea baada ya kuvunwa kutokana na miundombinu mibovu, ukosefu wa mafunzo na matumizi mabaya ya zana za uvuvi lakini serikali imekuja na mikakati ya kupunguza upotevu wa mazao hayo kwa kujenga miundombinu ya kuanikia samaki na dagaa maeneo ya Tanga, Kilwa, Bagamoyo, Mafia, Ziwa Tanganyika na Kigoma.
Aliongeza kuwa uvuvi wa bahari kuu unachangia asilimia 30 ya mazao ya uvuvi nchini ikilinganishwa na uvuvi wa maji baridi ambao unachangia asilimia 75 ambapo kwa Tanzania Watu milioni 4 wanategemea sekta ya uvuvi huku watu 200, 000 wakinufaika moja kwa moja na sekta hiyo.
Lengo la Warsha hiyo ambayo inafanyika kwa Siku tatu kuanzia Oktoba 7 hadi 9, 2025 ni kuleta pamoja wadau wa sekta ya uvuvi na bioanuai ili kujadili, kupanga na kuandaa Mpango wa Utekelezaji wa ujumuishaji wa bioanuai katika usimamizi wa uvuvi kwa kuzingatia Mpango wa Kimataifa wa Bioanuwai (GBF) na Mkakati wa Taifa wa Bioanuwai (NBSAP 2025-2030).