Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
AJENDA YA AKINAMAMA KWENYE SEKTA YA UVUVI, YAPEWA JICHO LA KIPEKEE KUKUZA UCHUMI
AJENDA YA AKINAMAMA KWENYE SEKTA YA UVUVI, YAPEWA JICHO LA KIPEKEE KUKUZA UCHUMI
Serikali imesema itaendelea kuiweka ajenda ya akinamama kwenye Sekta ya Uvuvi kuwa miongoni mwa ajenda zitakazokuwa zikipewa kipaumbele kutokana na umuhimu wake katika kukuza uchumi wa nchi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede amebainisha hayo (05.11.2024) Mjini Kigoma, wakati akifungua mkutano mkuu wa pili wa Jukwaa la Akinamama Wanaojishulisha na Shughuli za Uvuvi nchini (TAWFA), ambapo amesema kwa kufanya hivyo akinamama wataweza pia kuchangia kipato katika kaya zao.
Dkt. Mhede ameongeza kuwa maafisa maendeleo ya jamii wana nafasi kubwa ya kutoa elimu juu ya vyama vya ushirika kwenye vikundi mbalimbali ikiwemo TAWFA ili wapate uelewa sahihi wa umuhimu wa vikundi hivyo.
“Tutaendelea kuiweka ajenda hii ya akinamama kwenye Sekta ya Uvuvi iwe miongoni mwa maeneo tunayoangalia kwa jicho la ziada kwa umuhimu wake na pia tunakiri tuna jukumu la kuwa katika sehemu hii kwa sababu ndiyo njia ya kuinua uchumi kwa akinamama na kaya wanazozisimamia.” Amesema Dkt. Mhede
Aidha, katika mkutano huo amekubali kuwa mlezi wa TAWFA na kwamba yuko tayari kuhakikisha jukwaa hilo linakuwa na tija katika kukuza Sekta ya Uvuvi nchini kwa kubainisha kuwa asilimia 50 ya shughuli za uvuvi duniani zinajumuisha akinamama kupitia minyororo mbalimbali ya kuongezea thamani ya mazao ya uvuvi.
Pia, ametaka uwepo wa matumizi sahihi ya teknolojia na miundombinu kwa kuwa mafunzo lazima yaende sambamba na mahitaji hayo ili kuwa na bidhaa bora zitokanazo na Sekta ya Uvuvi.
Akimwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, Afisa Maendeleo ya Jamii wa mkoa huo Bw. Msafiri Nzunuri amesema Mkoa wa Kigoma umekuwa ukiweka juhudi mbalimbali za kukabiliana na changamoto za masoko kwa mazao ya uvuvi na kwamba kumekuwa na mabadiliko makubwa yenye kuleta matumaini.
Bw. Nzunuri ameongeza kuwa ili tija iweze kuonekana katika Sekta ya Uvuvi hususan kupitia akinamama, mkoa umekuwa na utaratibu wa utekelezaji kuanzia ngazi ya chini ili kuwatia moyo hususan akinamama wanaojishughulisha na uvuvi mdogo wa dagaa.
Pia, amesema mkoa utaendelea kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kuwa watakuwa mstari wa mbele kwa kuibeba vyema ajenda ya kuwainua akinamama wanaojishugulisha na shughuli za uvuvi ili waweze kukuza vipato vyao kwa kuwa na masoko ya uhakika.
Naye Mratibu wa Mradi wa Kimataifa wa Uvuvi Mdogo nchini kutoka Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) Dkt. Oliva Mkumbo amesema shirika hilo limedhamiria kuendeleza uvuvi mdogo ili kupunguza umasikini kwa akinamama wanaojishughulisha na uvuvi huo.
Dkt. Mkumbo amefafanua kuwa kote duniani uvuvi mdogo umekuwa na mchango mkubwa katika Sekta ya Uvuvi na wengi ni akinamama, hivyo FAO inashughulikia mapungufu katika miongozo ya hiari ya uvuvi huo.
Aidha, FAO kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewezesha uwepo wa TAWFA na mafanikio mengine ni kuundwa kwa dawati la akinamama la kijinsia na uwepo wa mikopo na mitaji.
Mwenyekiti wa TAWFA Bi. Beatrice Mbaga akizungumza katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa pili wa jukwaa hilo, ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea kuwashika mkono kwa kusimamiwa ili waweze kufikia malengo waliyokusudia.
Bi. Mbaga ameongeza kuwa wanatambua mchango mkubwa wa wafanyakazi wa wizara pamoja na mikakati mbalimbali inayowekwa na wizara hiyo katika kukuza Sekta ya Uvuvi hivyo TAWFA itahakikisha inasimamia yote ambayo yako chini ya serikali.
Baadhi ya wanachama wa TAWFA wanaohudhuria mkutano huo wamekuwa wakitoa shuhuda mbalimbali namna wanavyonufaika kiuchumi kupitia jukwaa hilo ikiwemo mikopo na kuongeza mahitaji ya masoko kutokana na bidhaa wanazouza.
Wameomba jukwaa hilo kuendelea kupata ufadhili kutoka FAO na serikali ili akinamama waweze kujikwamua zaidi kiuchumu kupitia Sekta ya Uvuvi.
Mkutano mkuu wa pili wa Jukwaa la Akinamama Wanaojishulisha na Shughuli za Uvuvi nchini (TAWFA) unafanyika kwa siku nne Mjini Kigoma ambapo majadiliano mbalimbali yanafanyika ili kutatua changamoto zinazowakabili.