Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

SERIKALI YATUMIA TEKNOLOJIA KUDHIBITI UVUVI HARAMU UKANDA WA BAHARI KUU

Imewekwa: 11 August, 2025
SERIKALI YATUMIA TEKNOLOJIA KUDHIBITI UVUVI HARAMU UKANDA WA BAHARI KUU

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DFSA) imefanikiwa kudhibiti vitendo vya Uvuvi haramu kwenye ukanda wa Bahari Kuu wenye kilomita za mraba 223,000 kwa kutumia vifaa vilivyounganishwa kupitia teknolojia ya kisasa.

Hayo yamesemwa Agosti 07,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Emmanuel Sweke alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya kimataifa ya Nane Nane yanayoendelea kwenye Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

“Tuna mfumo wa kutambua meli zote kwa haraka ambao unatuwezesha kufahamu Meli ambazo hatuzitambui, hazijakata leseni au hazina vibali na kwa utaratibu meli yoyote ile iliyosajiliwa inapaswa kutoa taarifa saa 24 kabla ya kuingia baharini” Amesema Dkt. Sweke.

Aidha Dkt. Sweke amebainisha kuwa mamlaka yake imekuwa ikifanikisha jukumu hilo la ulinzi wa rasilimali za Uvuvi wa bahari kuu kwa kushirikiana na kamisheni ya Jodari ya Bahari ya Hindi na kamisheni ya bahari ya Hindi iliyopo nchini Mauritania ambayo hushirikiana nayo kufanya doria ya pamoja kwenye ukanda huo

“Nitumie fursa hii kuwashukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa jitihada zao za kukomesha uvuvi haramu kwenye ukanda huu wa bahari kuu na kwa kweli vitendo hivyo vimebaki kuwa historia” Amesema Dkt. Sweke.

Mamlaka ya kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu inasimamia ulinzi na uendelezaji wa rasilimali zake kupitia Sheria ya usimamizi na uendelezaji wa Uvuvi wa Bahari kuu ya mwaka 2020 ambayo imekuwa ni mfano wa kuigwa kwa ukanda wa kusini magharibi mwa bahari ya Hindi.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo