Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MIFUGO NA UVUVI VINARA NANE NANE 2025!

Imewekwa: 11 August, 2025
MIFUGO NA UVUVI VINARA NANE NANE 2025!

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefanikiwa kushika nafasi ya kwanza kwenye maonesho ya kimataifa ya Nane Nane 2025 kwa upande wa Wizara za kisekta ikifuatiwa na Wizara ya Kilimo iliyoshika nafasi ya pili.

Wizara hiyo imeibuka na ushindi huo baada ya kuongoza katika vigezo mbalimbali hali iliyochagizwa na maandalizi mazuri iliyofanya katika maonesho hayo huku kivutio kikubwa kikiwa ni Paredi ya Mifugo iliyoambatana na maonesho ya Ndege nyuki maalum inayotumika kwenye udhibiti wa Uvuvi haramu.

Akizungumza katika kilele cha Maonesho hayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mbali na kuipongeza Wizara hiyo kwa jitihada ilizochukua katika udhibiti wa magonjwa ya Mifugo kupitia utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo, ameielekeza kuhakikisha inaweka kituo cha Ugani kwenye viwanja vya Maonesho hayo jijini Dodoma ambavyo rasmi leo vimetambulishwa kwa jina la Dkt. John Samwel Malecela ili wananchi waendelee kunufaika na elimu ya masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya Mifugo na Uvuvi.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amemshukuru Rais Samia kwa kuiongezea Wizara yake bajeti kwa mwaka huu wa fedha ambapo amebainisha kuwa hatua hiyo imeiongeza ajira kwa watu wengi hususan wanawake na vijana.

Maonesho hayo ambayo kilele chake ni Agosti 08 ya kila mwaka yataendelea kwa siku mbili zaidi kwa mwaka huu ili kuwapa fursa watu wengi zaidi kwenda kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo