Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

DKT. MGANGA AKOSHWA NA MATUMIZI YA NDEGE NYUKI ULINZI WA RASILIMALI ZA UVUVI NCHINI

Imewekwa: 11 August, 2025
DKT. MGANGA AKOSHWA NA MATUMIZI YA NDEGE NYUKI ULINZI WA RASILIMALI ZA UVUVI NCHINI

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga amefurahishwa na teknolojia ya Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi inayotumiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye ukanda wa Ziwa Victoria.

Dkt. Mganga amebainisha hayo mara baada ya kufika kwenye banda la Wizara hiyo Agosti 02,2025 lililopo kwenye Maonesho ya kimataifa ya Nane Nane Nzuguni jijini Dodoma ambapo ameipongeza Serikali kwa kubuni mbinu hiyo ya kisasa ya ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi nchini.

“Kupitia teknolojia hii wavuvi haramu wanaweza kubainika kwa haraka na wepesi bila kutumia nguvu kubwa na kunakuwa na ushahidi tofauti na hapo awali ambapo watu wengi walikuwa wanakana kwa sababu hakukuwa na ushahidi” Amesema Dkt. Mganga.

Aidha Dkt. Mganga ameongeza kuwa uwepo wa teknolojia hiyo umesababisha kupungua kwa vitendo vya uvuvi haramu nchini jambo ambalo amesema kuwa litasaidia kuongeza kiwango cha samaki kwenye vyanzo vya asili.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Udhibiti Ubora Dkt. Christian Nzowa amesema kuwa Ndege nyuki hiyo ina uwezo wa kutembea hadi umbali wa kilomita 4 huku ikirekodi matukio yote yanayoendelea ziwani huku pia ikiwa na uwezo wa kubaini hatari yoyote inayojitokeza ziwani na kutuma ishara kwenye kituo cha uangalizi.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo