MAJALIWA ARIDHISHWA NA MAENDELEO SEKTA YA UFUGAJI SAMAKI

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameridhishwa na maendeleo ya Sekta ya Ufugaji wa samaki nchini ambapo amewataka wananchi kuelekeza nguvu kwenye tasnia hiyo ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa samaki nchini.
Mhe. Majaliwa ameyasema hayo Agosti 03, 2025 mara baada ya kufika kwenye eneo la mabwawa ya ufugaji samaki na vizimba lililopo kwenye banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikiwa ni sehemu ya Maonesho ya kimataifa ya Nane Nane yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
“Mhe. Rais amesambaza vizimba vingi vya kutosha kanda ya ziwa, nilitaka kufahamu kama tumefanikiwa” amesema Mhe. Majaliwa.
Aidha Mhe. Majaliwa ameridhishwa na gharama ya vizimba hivyo ambayo amekiri hata watu wa kipato cha chini wanaweza kuimudu huku pia akitoa rai kwa wananchi wote hususani wadau wa Uvuvi kutumia zana zilizoidhinishwa na Serikali wakati wote wa utekelezaji wa shughuli zao za Uvuvi.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wenzake wa mkopo wa masharti nafuu wa vizimba hivyo Makamu mwenyekiti kutoka kikundi cha Vijana Kazini kutoka mkoani Mwanza Bw. Elisha Gayo ameishukuru Serikali kwa mkopo wa shilingi milioni 117 waliopatiwa ambapo amekiri umesaidia kubadili maisha yao kwa kiasi kikubwa.