CHANJO NA UTAMBUZI NI MAPINDUZI YA SEKTA YA MIFUGO NCHINI-DKT.KIJAJI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo itakuwa ni chachu ya mapinduzi wa sekta ya Mifugo nchini.
Mhe. Kijaji amesema hayo wakati wa ziara yake ya Ukaguzi wa utekelezaji wa kampeni hiyo Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro Julai 10, 2025 ambapo amebainisha kuwa kufanyika kwa kampeni hiyo kunaweka ukomo wa kutorosha mifugo katika nchi jirani ambako wafugaji walikuwa wanaenda kutafuta masoko kwenye nchi zilizopata ithibati ya Shirika la kimataifa la Afya ya wanyama (WOAH).
“Kwa hivi sasa baada ya kutangaza tu kuanza kwa kampeni hii tayari masoko ya kimataifa yameonesha dhamira ya kuhitaji Mifugo yetu hai na mazao yake na ninatamani itakapomalizika miaka 5 ya utekelezaji wa kampeni hii turejee kwa Mhe. Rais na kumuonesha namna alivyofanikiwa kubadili sekta yetu ya Mifugo” Ameongeza Mhe. Dkt. Kijaji.
Akielezea ubora wa hereni za kielektroniki zinazotumika kwenye zoezi la Utambuzi wa Mifugo, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini Dkt. Benezeth Lutege amesema kuwa hereni hizo zimetengenezwa kwa kuzingatia ustawi wa wanyama ikiwa ni pamoja na kuwekewa kifaa maalum kinachoziwezesha kuzunguka sikioni pindi mnyama anapotembea.
“Lakini pia hereni hizi mbali na kuwa na gamba gumu lisiloweza kuvunijika, maandishi yake yameandikwa kwa mionzi mikali na hivyo kutoweza kufutika hata yakikwanguliwa na kifaa chenye ncha kali” Ameongeza Dkt. Lutege.
Akizungumza kwa niaba ya wafugaji wa Mkoa wa Morogoro, Kiongozi wa kimila wa mikoa ya kanda ya Mashariki Chifu Kashu Moreto amesema kuwa chanjo hizo na hereni zinafuta fikra potofu waliyokuwa nayo wafugaji hapo awali ambapo waliamini mifugo inachanjwa na kutambuliwa ili itaifishwe na Serikali.
“Kwa bahati nzuri Rais wetu mpendwa ameongea maneno mazuri kwa kusema hereni zitatolewa bure hivyo mimi kwa kuwa ni kiongozi wa takribani mikoa 7 hivyo nitapiga kelele kwa wafugaji wenzangu wote tukachanje ila naomba Serikali iendelee kusimamia vema zoezi hili ili chanjo hizo ziendelee kuwa salama kwa Mifugo yetu” Amesema Chifu Kashu.
Ziara hiyo ya Mhe. Dkt. Kijaji iliyolenga kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo iliyozinduliwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Juni 16, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inatarajiwa kuhitimishwa katika Wilayani Bahi mkoani Dodoma.