BUNGE LAIDHINISHA BAJETI YA TSH. BIL.476.6 WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI

BAJETI ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewasilishwa bungeni huku mafanikio lukuki yaliyopatikana kwenye sekta za mifugo na uvuvi ndani ya kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita yakibainishwa na hatua kadhaa zikitajwa kuchukuliwa na wizara kwa lengo la kuziwezesha sekta hizo muhimu kuendelea kuwa na mchango zaidi kwenye Pato la Taifa (GDP).
Akiwasilisha bajeti hiyo yenye muelekeo wa kuongeza uzalishaji na kukuza masoko ya mazao ya mifugo na uvuvi, bungeni jijini Dodoma Mei 23, 2025, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amebainisha mafanikio kadhaa ambayo sekta za mifugo na uvuvi zimeyapata.
Dkt. Kijaji akihutubia bunge hilo alisema kuwa moja ya mafanikio makubwa ambayo wizara yake imeyapata ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuongezeka kwa bajeti ya wizara kutoka Shilingi Bilioni 295.5 Mwaka 2023/2024 hadi Shilingi Bilioni 476.6 Mwaka 2025/2026 hatua ambayo inatafsiri kinagaubaga dhamira ya dhati ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha sekta za mifugo na uvuvi zinaendelea kuwa chachu ya uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.
Ameongeza kwa kusema kuwa utekelezaji wa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) imewezesha jumla ya vikundi 20 vyenye vijana 106 kupatiwa ekari 1,761 katika Ranchi ya Kagoma na kupewa mkopo usio na riba wa jumla ya shilingi 934,231,000 kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa ajili ya kuendesha shughuli za unenepeshaji ng’ombe. Vijana hao walianza kazi ya unenepeshaji wa ng’ombe Januari, 2025 ambapo hadi kufikia Aprili, 2025 jumla ya ng’ombe 627 wenye thamani ya shilingi 451,440,000 walinunuliwa na kunenepeshwa kwa wastani wa shilingi 720,000 kwa kila ng’ombe, na kati ya ng’ombe hao, 452 waliuzwa kwa wastani wa shilingi 890,000 kwa kila ng’ombe na kupatikana kwa faida ya shilingi 76,840,000 ikiwa ni wastani wa shilingi 170,000 kwa kila ng’ombe.
Ameendelea kufafanua kuwa, hatua ya kupumzisha shughuli za uvuvi Ziwa Tanganyika umepelekea mavuno ya samaki kuongezeka katika ziwa hilo kufikia tani 38,999.82, zenye thamani ya shilingi 324,845,566,002.38 katika kipindi cha miezi minne (4) baada ya kufungua Ziwa kati ya Mwezi Septemba hadi Desemba, 2024 ikilinganishwa na tani 25,113.43, zenye thamani ya shilingi 166,476,911,002.19 kwa kipindi kama hicho Mwaka 2023 kabla ya kupumzisha Ziwa. Kutokana na ongezeko hilo imepelekea kiasi cha mazao ya uvuvi yaliyouzwa nje ya nchi kutoka Ziwa Tanganyika kwa Mwaka 2024 kuongezeka kufikia tani 1,227.21 zenye thamani ya shilingi 180,684,608,011.64 ikilinganishwa na tani 664.11 zenye thamani ya shilingi 97,036,183,747.23 Mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko la asilimia 84.79.
Mafanikio mengine ambayo Dkt. Kijaji ameyataja ni kuondoa uvuvi haramu wa kutumia vilipuzi (blast fishing) katika Ukanda wa Bahari ya Hindi ambapo kwa sasa hali hiyo imedhibitiwa kuanzia vyanzo, wasambazaji na watumiaji wa vilipuzi na kwa zaidi ya mwaka hakuna matukio ya uvuvi huo kwa ukanda wote wa Bahari ya Hindi.
Ameongeza kwa kusema kuwa wizara yake imeweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji ili uhalifu huo usiendelee siku zijazo huku akibainisha kuwa kwa upande wa Maziwa Makuu wizara yake inaendelea na kazi ya kusafisha na kuondoa zana haramu za uvuvi jambo ambalo limesaidia kugundua na kunasa mtandao mpana wa uingizaji wa nyavu haramu. Mafanikio yote yanayopatikana yanatokana na ushirikishwaji thabiti wa wadau mbalimbali wa Sekta ya Uvuvi wakiwemo Viongozi wa Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi na Asasi Zisizo za Kiserikali (NGO).
Katika hatua ya kuhakikisha kunakuwa na usalama wa chakula na lishe, Dkt. Kijaji amesema katika kipindi cha miaka minne wizara yake imeendelea kupandikiza vifaranga vya samaki katika maeneo mbalimbali nchini ambapo hadi sasa jumla ya vifaranga 2,699,630 vya samaki, vyenye thamani ya Shilingi 269,963,000 vimepandikizwa katika Ziwa Ikimba (2,000,000) - Bukoba na mabwawa mawili (2) yaliyopo - Mufindi – Bwawa la asili la Nzivi (300,000) na Bwawa la Kihanga (300,000); Igunga - Bwawa la Mwamapuli (13,830); Ngara (1,000), na Lushoto - Bwawa la Gereza la Lushoto (60,000); Shule ya Irente (3,000); Sekondari ya Magamba (1,800) na Bwawa la kikundi cha Ngulwi (20,000).
Aidha, Dkt. Kijaji amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne, wizara yake imeendelea na utekelezaji wa mradi wa kutoa mikopo isiyo na riba na yenye masharti nafuu wa kuwezesha wananchi vizimba vya kufugia samaki na pembejeo zake katika mikoa ya Mara, Simiyu, Mwanza, Kagera, Geita, Katavi, Rukwa na Kigoma huku akibainisha kuwa hadi kufikia Aprili 2025 vizimba 480 vimekopeshwa kwa wanufaika 1,338 na jumla ya tani 216.68 za samaki zenye thamani ya Shilingi 1,576,132,969.36 zimevunwa kwenye vizimba 157 vya vikundi 32 na kufanya marejesho ya Shilingi 1,528,734,615.66.
Pia, Dkt. Kijaji ameongeza kuwa kwa mara ya kwanza, Serikali inakwenda kuzindua na kutekeleza Kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo nchi nzima lengo likiwa ni kuboresha afya ya mifugo na kuiongezea thamani ili iweze kuuzika kwenye masoko ya kimataifa.
Dkt. Kijaji ameendelea kuweka wazi kuwa Wizara yake kupitia Bodi ya Nyama imeendelea kutekeleza mkakati wa kukuza mauzo ya nyama nje ya nchi kwa ajili ya kuongeza fedha za kigeni huku akibainisha kuwa hadi kufikia Aprili 2025, jumla ya tani 9,863.41 za nyama zenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.7 zimeuzwa sawa na asilimia 89.9 ya lengo la kuuza tani 10,971 ikilinganishwa na tani 9,326.3 zenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.4 zilizouzwa kipindi kama hicho katika Mwaka 2023/2024. Ongezeko hili ni sawa asilimia 5.75 Hii ni kutokana na jitihada zinazofanywa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongeza ushirikiano na fursa za kibiashara nje ya nchi iliyopelekea masoko ya nyama kuendelea kuongezeka kufikia nchi 11 ambazo ni Bahrain, Comoro, Hong Kong, Jordan, Kenya, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Vietnam.
Vilevile, Dkt. Kijaji hakusita kueleza hatua za ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko ambao wizara yake unaendelea kuutekeleza na kuweka wazi kuwa hadi kufikia mwezi Aprili, 2025 ujenzi huo umefikia asilimia 81.9. na kwamba katika hatua hizo za ujenzi umeshatoa ajira kwa wananchi takriban 570, na utakapokamilika unatarajiwa kuajiri zaidi ya watu 30,000.
Mafanikio mengine aliyoeleza Dkt. Kijaji ni kuongezeka kwa ulaji wa nyama, mayai na maziwa kwa wananchi kutokana na kuimarika kwa biashara ya mazao ya mifugo nchini kwa Mwaka 2024/2025. Akifafanua, Dkt. Kijaji amesema kiwango cha unywaji wa maziwa kwa mtu mmoja kimeongezeka kutoka wastani wa lita 67.5 Mwaka 2023/2024 hadi lita 68.1 Mwaka 2024/2025, ulaji wa nyama kutoka kilo 16 Mwaka 2023/2024 hadi kilo 17.6 Mwaka 2024/2025 na ulaji wa mayai kutoka 107 Mwaka 2023/2024 hadi 119 Mwaka 2024/2025. Aidha, ameongeza kuwa pamoja na ongezeko hilo, ulaji wa mazao hayo kwa mtu mmoja mmoja bado haujafikia viwango vinavyopendekezwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ambavyo ni lita 200 za maziwa, kilo 50 za nyama na mayai 300.
Hatua nyingine ya muhimu ambayo Dkt. Kijaji amebainisha ni kudhibitiwa kwa magonjwa yaenezwayo na kupe, mbung’o na wadudu wengine kwa kuratibu uogeshaji wa mifugo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa huku akisema kuwa hadi kufikia Aprili 2025, jumla ya michovyo 1,337,306,118 ya mifugo ikijumuisha ng’ombe 619,731,619, mbuzi 497,805,601, kondoo 198,572,994 na punda 21,195,904. Aidha, amefafanua kuwa uogeshaji huo wa mifugo umesaidia kupunguza matukio ya vifo vya mifugo nchini kutoka asilimia 48 ya vifo vyote katika Mwaka 2023/2024 hadi asilimia 45 kufikia Aprili, 2025.
Kama hiyo haitoshi, Dkt. Kijaji ametaja vipaumbele vinne (4) ambavyo wizara yake imekusudia kuvitekeleza ili kuendeleza mapinduzi makubwa katika sekta za mifugo na uvuvi, vipaumbele hivyo ni pamoja na kuongeza uzalishaji, thamani, na masoko ya mazao ya mifugo na uvuvi, Kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za mifugo na uvuvi, Kuhamasisha uwekezaji kwenye Sekta za Mifugo na Uvuvi, na Kuimarisha utafiti, mafunzo na huduma kwa sekta za Mifugo na Uvuvi.
Aidha, Dkt. Kijaji alitumia hotuba yake ya bajeti kupongeza jitihada binafsi zinazofanywa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kuziwezesha sekta za mifugo na uvuvi kuongeza tija katika uzalishaji na kukuza masoko ili kuifanya wizara kuwa na mwelekeo wa kibiashara zaidi ili kufanya wingi wa rasilimali zilizopo ziendane na mchango sawia katika pato la taifa.