​ZOEZI LA UTAMBUZI WA MIFUGO LILETE TIJA KWENYE UZALISHAJI

Imewekwa: Saturday 11, June 2022

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Mej. Jen. Suleiman Mzee amewataka Wataalam wa Mifugo wa Jeshi hilo kutumia Mafunzo ya Usajili na Uwekaji wa alama za Utambuzi wa Mifugo kwenda kuongeza tija ya uzalishaji katika maeneo wanayotoka.

Kamishna Jenerali Mzee ameyasema hayo leo (10.06.2022) wakati akifungua Mafunzo ya Usajili na Uwekaji wa alama za Utambuzi wa Mifugo kwa Wataalam wa Mifugo wa Jeshi la Magereza yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Meja Jenerali Suleiman Mzee - Msalato Jijini Dodoma.

“Usajili na Uwekaji wa Alama za Utambuzi kwa mifugo inayomilikiwa na Jeshi la Magereza kutasaidia Jeshi kuwa na taarifa sahihi za idadi ya mifugo ikiwa ni pamoja na kulinda mifugo hiyo,” alisema

Jeshi la Magereza limekuwa likipata changamoto ya taarifa sahihi za uzalishaji wa mifugo na mazao yake, hivyo kwa kutumia njia hii ya usajili na utambuzi kutasaidia sana hata kwenye usimamizi wa uzalishaji wa mifugo pamoja na mazao yake.

Aidha, amewapongeza waataalam hao wa mifugo kwa kazi nzuri ambayo wanayoifanya kwani kwa sasa mifugo katika Jeshi hilo imeanza kuongezeka. Vilevile amewasihi wataalam hao kuhakikisha wanaongeza jitihada zaidi katika usimamizi wa uzalishaji wa mifugo na mazao yake. Pia amewataka wataalam hao pamoja na viongozi wao kwenye maeneo wanayotoka kuongeza ubunifu katika uzalishaji.

Naye Afisa Utambuzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo), Dkt. Gibonce Kayuni amesema kuwa usajili na utambuzi wa mifugo kwa njia ya kielektroniki una faida nyingi ikiwemo ya kuwa na taarifa sahihi za takwimu za mifugo kitu kitakachosaidia katika upangaji wa mipango ya maendeleo ya mifugo. Pia zoezi hili litasaidia kupunguza tatizo la wizi wa mifugo na kuwawezesha wafugaji kupata bima itakayowawezesha kukopesheka kwenye taasisi za fedha.

Mkurugenzi wa Sehemu ya Kilimo, Mifugo na Utunzaji wa Mazingira, ACP. Rocky Mbena amesema kuwa kwa sasa Magereza inaendelea na uboreshaji wa Kosaafu za Mifugo ili kuwa na mifugo itakayozalisha kwa tija. Lakini pia wanaendelea na uboreshaji wa mahusiano na wadau mbalimbali wa mifugo kwa lengo la kuongeza tija kwenye uzalishaji.

.
Tanzania Census 2022 Tanzania Census 2022