WATAKAOSHINDWA KUSAJILI MIFUGO KWA HIYARI KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA

Imewekwa: Monday 03, January 2022

Serikali imesema itawachukulia hatua wafugaji watakaoshindwa kusajili mifugo yao kwa njia ya utambuzi wa hereni za kielekroniki pindi zoezi hilo litakapofungwa agosti 2022.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na Ustawi wa Wanyama, Dkt. Annette Kitambi wakati wa utoaji mafunzo ya utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielekroniki Disemba 21,2021 Mkoani Morogoro.

Alisema kwa sasa zoezi hilo linaendelea kwa utoaji elimu kwa wataalam na viongozi kutoka Serikali za mitaa ngazi ya mkoa na wilaya pamoja na wafugaji ambao kwa pamoja watahusika katika kutekeleza zoezi hilo linalotarajiwa kuanza mapema Januari mwakani.

"Sheria zipo lakini kwa sasa hivi tunafanya kwa kuwahamasisha na kuwaelimisha, zoezi hili litaenda mpaka agosti mwakani tutakuwa tumemaliza kwa hiyari ndipo sheria zitaanza kutumika na sheria imeweka wazi kwamba ikibainika haijatambulika utapigwa faini ya shilingi milioni 2 au kwenda jela miezi sita au vyote kwa pamoja" alisema

Akisoma hotuba kwa niaba ya mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo hayo Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Mhandisi Ezron Kilamhama akawataka wakuu wa Wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo kuhakikisha wanasimamia ipasavyo zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielekroniki.

Alisema zoezi hilo linaloenda na utoaji elimu kwa watendaji wa serikali ngazi ya halmashauri ni vyema kwa wataalam kila mmoja akaelewa vizuri muongozo, sheria na kanuni ili aweze kwenda kutoa elimu kwa wafugaji na wataalam waliopo ngazi za chini.

"Niwaagize wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuhakikisha elimu hii inayotolewainawafikia wafugaji na kuhakikisha mifugo yote iliyoainishwa kwenye muongozo ambayo ni Ng'ombe, Punda, Mbuzi na kondoo inavalishwa hereni katika maeneo yenu" alisema.

.
Tanzania Census 2022 Tanzania Census 2022