​WAFUGAJI WILAYANI HANDENI WAHIMIZWA KUFUGA KIBIASHARA

Imewekwa: Tuesday 10, May 2022

Wafugaji wa Wilaya ya Handeni wamehimizwa kufuga biashara ili waweze kuongeza kipato katika familia zao kutokana na shughuli za ufugaji wanazofanya.

Hayo yamesemwa (29.04.2022) na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ugani, Bi. Felista Kimario wakati wa mafunzo yaliyotolewa kwa wafugaji hao katika vijiji vya Mkata, Mazingara, Gendagenda na Kwasunga wilayani Handeni mkoani Tanga ambapo wizara ya Mifugo na Uvuvi upande wa Sekta ya Mifugo imeendesha mafunzo hayo kwa ajili ya kuwajengea uwezo wafugaji hao.

Bi. Kimario amesema kuwa wizara imekuwa ikitoa elimu kwa wafugaji katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kuhakikisha wafugaji wanafuga kibiashara na kukuza kipato chao. Wafugaji wengi bado wamekuwa wakiendelea na ufugaji wa mazoea hali inayosababisha wafugaji hao kuwa na mifugo mingi ambayo haiwasaidii sana katika kuongeza kipato katika familia zao na taifa kwa ujumla.

“Elimu tunayoitoa hapa itawasaidia wafugaji hawa kuelewa nini maana ya ufugaji wa kibiashara, umuhimu wa uanzishaji wa mashamba ya malisho kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la malisho, udhibiti wa magonjwa ya mifugo, matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa utoaji huduma za ugani (M-KILIMO), umuhimu wa mashamba darasa, umuhimu wa wafugaji kujiunga kwenye ushiriki na matumizi ya hereni za kielektroniki,” alisema

Bi. Kimario aliongeza kuwa wafugaji wanapopata elimu hii pamoja na mada nyingine na wakaifanyia kazi ni lazima kutakuwa na mabadiliko makubwa kwenye sekta ya mifugo. Wafugaji wanatakiwa kuamua kubadilika na kufuga kulingana na ushauri wanaopatiwa na wataalam ili wafuge kwa tija.

Naye Selemani Nyauba ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwasunga amesema kuwa kupitia elimu hii wameweza kuelewa umihimu wa upandaji wa malisho kwa wafugaji kitu ambacho kitasaidia kuondokana na migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi hususani wakulima wakati malisho ya asili yanapokosekana. Hivyo amewasihi wafugaji kuona namna ya kuanza kutekeleza hili. Vilevile kuhusu suala la hereni za kielektroniki amesema kuwa ni jambo zuri ambalo litasaidia sana kupunguza tatizo la kesi za wizi wa mifugo ambazo zilikuwa zikiripotiwa ofisini kwake.

Aidha, ameiomba wizara kuendelea na utaratibu huo wa kuwatembelea wafugaji na kuwapatia elimu kwa kuwa inawasaidia kujifunza mambo mengi sana yanayohusu ufugaji wa kisasa.

Naye Hamza Masimba ambaye ni mfugaji katika Kijiji cha Gendagenda wilayani humo ameishukuru wizara kwa kuwapelekea mafunzo hayo ambayo yamewasaidia kufahamu mambo mengi kuhusu ufugaji ambayo mengi walikuwa hawayafahamu. Aidha, kutokana na mafunzo hayo wametambua kuwa ni muhimu sana kuwatumia wataalam wa mifugo walionao pamoja na Mfumo wa M-KILIMO katika kutatua changamoto za ufugaji wanazokutana nazo.

.
Tanzania Census 2022 Tanzania Census 2022