TEKNOLOJIA YA USALAMA NA UOKOZI YATAJWA KUSAIDIA WADAU WA UVUVI

Imewekwa: Friday 29, October 2021

Serikali imesema kuwasilishwa kwa teknolojia ya usalama na uokozi kwa wadau wa sekta ya uvuvi kutasaidia kuzuia utoroshaji wa mazao ya uvuvi pamoja na kukusanya maduhuli.

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi amebainisha hayo jijini Dodoma wakati wa kupokea wasilisho la awali kutoka kwa shirika lisilokuwa la kiserikali la Tanzania Agricultural Business Company Ltd (TABCO), juu ya teknolojia ya usalama na uokozi.

Bw. Bulayi alisema endapo teknolojia hiyo ikieleweka vyema na hatimaye kutumika na wadau wa Sekta ya Uvuvi itasaidia ukusanyaji wa maduhuli kutokana na mwenendo wa chombo cha uvuvi kwa kuwa chombo hicho kitakuwa kikionekana kupitia setilaiti.

Aliongeza kuwa ili utekelezaji wa teknolojia hiyo uweze kufikia malengo ni lazima wavuvi wao wenyewe kufuata sheria na kwamba wasilisho hilo lipo katika hatua ya awali na endapo likikamilika wizara na taasisi nyingine za serikali zitaweka utaratibu ambao utakubalika kwa wadau wote ili kusaidia kutekeleza majukumu yakiwemo ya kulinda rasilimali za uvuvi.

Pia alisemateknolojia hiyo itasaidia kufahamu wakati ambao mvuvi akipata dhoruba akiwa majini na kuweza kumpatia msaada kwa haraka zaidi.

.